Katika maisha usiziangalie Changamoto, angalia faida iliyoko mbele ya changamoto, zingatia furaha utakayoipata baada ya changamoto.

Bila shaka wengi wetu huwa tunalisikia neno ‘Changamoto’ lakini sina hakika kama ni wote tunafahami nini hasa uhalisia au maana yake. Leo naomba nijaribu kuliweka hili sawa kwa kwa tafsiri isiyo rasmi kwamba Changamoto ni kitu chochote kitachoweza kutikisa akili (fikra) ya binadamu yeyote.

Changamoto pia ni matukio ambayo humfika binadamu kwa nyakati tofauti katika maisha yake ya kila siku kwa kusudi la kumfundisha au kumtoa sehemu fulani ya maisha na kumpeleka sehemu nyingine kwa namna tofauti, kwa kifupi tunaweza sema Changamoto jirani yake ni mafanikio.

Zipo changamoto za aina nyingi na zina majina mengi tofauti mfano matatizo, shida, magonjwa, mitihani ya maisha, migogoro n.k kama ambavyo hii leo nataka tujifunze kitu kupitia Bwana mmoja aitwaye Makau Chilangazi, ambaye ni kijana mwenye umri wa miaka 27, lakini mazonge aliyokutana nayo yanamfanya kuonekana shujaa mbele ya changamoto.

Safari ya Maisha.

Kutokana na jina lake la la pili la Chilangazi, wengi waliamua kufupisha na kumuita Chila ikiwa ni kisifa kutokana na uwezo wake wa kutumia akili kuamua kufanya au kutenda jambo fulani ambalo halikumpelekea mwisho wake kuwa wa majuto, alifanya mambo ya tofauti na matarajio ya wengi, pale ambapo alikutana na changamoto mbalimbali za maisha.

Katika safari yake ya maisha, wakati fulani akiwa katika mihangaiko yake ya kiuchumi, Chila alifanikiwa kulima zao la Mahindi na Alizeti, Shamba lake lilizungumziwa na kila mtu aliyepita jirani kutokana na afya ya mimea kiasi watabiri kudai tayari Chila ameuaga umasikini endapo ataamua kuendeleza Kilimo cha biashara.

Habari zilimfikia Chila, kiasi akawa anajiwazia moyoni jinsi ya kujianzishia biashara ya ziada ili kujikuza kiuchumi, “nikifungua salon ya kiume natafuta kijana namuweka hapo, halafu natafuta kijana mwingine anauza chips, kisha namtafuta mama wa makamo naanzisha biashara ya chakula sina shaka mwanzo mzuri nitafanikiwa,” alijiwazia Chila.

Kifo cha Baba.

Wakati huu akiwa amezama katika lindi la mahesabu, simu yake ilikuwa imeita si chini ya mara sita lakini hakuipa umuhimu kwani alizama sana katika fikra za kimahesabu na kibiashara, ila hodi ya mlangoni pake ilimshtua akaenda kufungua huku akijiuliza ni nani usiku ule, kumbe alikuwa ni mke wa Mzee Matata, mlanguzi wa mazao ya Wakulima.

Moyoni alijisemea tayari Mzee Matata anaanza kuja kumlaghai, lakini Mama huyo kwa upole alimsalimia Chila na kumpa pole, na wakati Chila anashangaa ni pole ya kitu gani yule Mama akaendelea, “Mzee ameniagiza nije nikuambie uwe na moyo mkuu lakini pia utulie wakati yeye anakuja, ili mjue cha kufanya na maandalizi ya msiba.

Kwa haraka bila kujibu chochote Chila alikumbuka kwamba simu yake ilikuwa ikiita na haikuipa kipaumbele, hivyo akaikimbilia kwa kasi na alipoishika alikuta misimbo 16 ya simu isiyojibiwa, hivyo alitaka kujua ni nani?. Jina la kwanza lilikuwa ni la Mjomba wake Madewa, la pili ni Dada yake Regina na tatu alikuwa jirani yake Kajola.

Wakati akitaka kumtafuta Mjomba wake aliona kibahasha juu ya kioo cha simu yake, kufungua ulikuwa ni ujumbe kutoka kwa mama yake akimtaarifu kifo cha Baba yake, Chila alichanganyikiwa maana hakusikia taarifa za kuugua kwa mzazi wake zaidi jioni alipowasiliana naye alitaarifiwa kuwa ataenda kuwinda kama ilivyo ada.

Taarifa za kina za kifo cha Baba yake alizipata baada ya Mzee Matata alipofika nyumbani kwake kumpa pole, alizungumza naye na kumtaarifu kuwa alivamiwa na kundi la Simba wakati akikaribia pori la akiba alipokuwa akiwinda na hivyo taratibu za mazishi zilianza katika Kijiji hicho cha Sanza Kilichopo Wilayani Manyoni na hatimaye walimaliza msiba salama.

Maamuzi sahihi.

Wakati wa shughuli za msiba Chila ilimlazimu kumkopa kiasi cha pesa rafiki yake Mbega akimuahidi atamlipa baada ya mavuno, safari hii hakuwaza tena kuhusu biashara bali aliwaza namna ambavyo atalipa deni la rafiki yake na kiasi kitakachobaki kiweze kumudu kuendesha maisha yake na uangalizi wa familia aliyoachiwa na mzee wake.

Baada ya kuvuna, alilipa deni na kiasi kingine aliona ni vyema akazalisha ili kimsaidie kumudu gharama za maisha, hivyo aliazimia kuanzisha biashara ya mafuta ya kuendeshea vyombo vya moto akianza na mtaji wa lita 40, ambazo alikuwa akipima kwenye chupa na kuuza rejareja. Alifanikiwa kwa awamu ya kwanza hivyo kufurahia akiona alifanya maamuzi kwa wakati sahihi.

Kisicho riziki hakiliki.

Siku moja akiwa amerudi Sanza kutoka Manyoni mjini kuchukua bidhaa, alihisi kuwa na njaa, hiyo ilikuwa ni jioni hivyo aliona ni bora afikishe madumu yale nyumbani kwanza ambapo wazo lilimjia baada ya kufika kwamba awashe moto abandike chungu cha ugali kisha aende gengeni kununua Maharage ya kupima, alifanikiwa.

Alimkuta mama muuzaji wakabadilishana mawili matatu kuhusu maisha na kisha alipimiwa hitaji lake akalipa shilingi 500 lakini kabla hajaondoka walishtushwa na kelele kutoka upande wa Kaskazini aliotokea Chila, …. Moto… jamani moto… majirani….. Chila alikimbilia ule upande kutoa usaidizi lakini kila alivyojaribu kusogea alikuwa akikaribia kwake, kumbe moto ulishika yale madumu ya Mafuta na kulipua nyumba.

Ama kweli, Ng’ombe wa masikini hazai… alijiwazia Chila maana juhudi zake zote ziligonga mwamba akaanza kuhisi mambo mbalimbali kila alipojiuliza lakini akapiga moyo konde. Siku hiyo alipata hifadhi kwa jirani bila lepe la usingizi na kesho yake alianza kusuka upya kibanda chake kwa msaada wa vijana wenzie, ili aweze kujisitiri maana alipoteza kila kitu na hakuwa na pesa ya ziada. Chila alikumbuka msemo wa Wahenga kuwa ” Kisicho riziki hakiliki” na kisha alimshukuru MUNGU.

Shetani yupo kazini.

Miezi ilipita, akiwa hana hili wala lile pale Kijijini zaidi ya kuganga njaa na siku moja wakaja wageni kutoa Semina ya afya magonjwa kuambukiza. Kati ya waliojitokeza Chila alikuwepo na baada ya kumalizika kwa semina wageni wale waliondoka lakini baada ya muda walirejea wakidai wamepotelewa na simu. Wakati upekuzi ukifanyika simu ilikutwa katika dawati alilokuwa amekaa Chila.

Watu walimsakama kwa aibu ile wakidai sasa wanaishi na mwizi kijijini pao, alijitetea lakini hakueleweka na jamii na ilimbidi kutumia kila ushawishi na wageni wale waliona heri nusu shari maana simu waliipata na wakaondoka, lakini huku nyuma Chila aliendelea kusakamwa lakini yeye hakuwajibu vibaya zaidi aliwasihi na kuwaelekeza kuwa hakuiba wala kugusa na hajui kilichotokea mpaka simu kufika pale, hilo halikusaidia kiasi alijiseme moyoni kuwa “Shetani yupo kazini”.

Ukubwa matukio.

Jamii ilimtenga Chila, akajiona hafai kila anapotokea watu wanakaa kwa tahadhari. Alipewa jina la mwizi na watu walianza kuunganisha matukio wakadai ndiyo maana hafanikiwi na hata moto uliunguza kibanda chake kwa kuwa alidhulumu watu, hakuna aliyekumbuka jema la kwake hata moja, aliwaza sana lakini alishtushwa na sauti ya binti aliyemsogelea ambaye kwanza alimsonya kisha alimwambia ana ujauzito wake na ajiandae kuwa baba mwizi mwenye mtoto jambazi.

Chila hakukasirika, kwa mbali alisikia sauti ikimuambia “Ukubwa matukio” alinyamaza kwa muda na kisha alitikisa kichwa kumaanisha alikubali matokeo na alimsihi Binti yule amuache apambane kwa ajili yake na mwanaye, huku akimuambia suala la wizi ni maneno tu ya watu. Miezi ilikatika na hatimaye binti alishikwa na uchungu na lipofika Zahanati alijifungua salama mtoto wa kiume lakini kutokana na kupoteza damu nyingi wakati wa uzazi Binti yule aliaga dunia na kuacha kichanga, Chila alilia.

Hapo kasheshe likaanza kwa Wazazi wa binti aliyefariki kudai Chila hakufuata taratibu na alitakiwa kuwajibika kwa kifo cha mtoto wao. Ilibidi wazee waingilie kati sakata hilo na busara zikatumika la sivyo hali ingekuwa mbaya kwa Chila. Hakuwa na kazi, hana kipato, Jua lilikuwa kali na kila alichojaribu kufanya kilishindikana hivyo akapata wazo la ziada ambalo alihisi ni suluhisho lake la mwisho.

Siku ya kufa Nyani.

Aliazimia kwenda kwa Binamu yake ambaye alikuwa akiishi Kijiji cha Chikuyu kiliochopo barabara kuu ya Manyoni – Dodoma, siku ya safari aliomba lifti ya Pikipiki kwa msambazaji haramu wa Mkaa, ili afike haraka kuomba msaada na ushauri ni namna gani angeweza kulea mtoto ambaye alimuacha kwa mama yake Sanza na angalau apate kitu cha kufanya, lakini wakati akiwaza hayio njiani Mvua kubwa ilianza kunyesha na kupelekea barabara kujaa maji na utelezi na mbeleni walipata ajali.

Kweli siku ya kufa Nyani Miti yote huteleza. Hata hivyo Chila hakuumia lakini Dereva Pikipiki alivunjika mguu, habari kufika Kijijini minong’ono ikatawala kwamba huenda hata alisababisha ajali makusudi ili apore Pikipiki ya watu, kitu ambacho alikikanusha lakini hakueleweka. Alikosa amani na aliazimia kutorudi tena Sanza kwani watu walimtumia ujumbe kuwa asijaribu kurudi, hivyo alimuandikia mama yake ujumbe wa simu na alimuahidi kupambana popote atakapoenda.

Wakati huu hakuwa na la kufanya na hakujua sasa ataenda wapi huku wazo la kwa Binamu yake akiliona halina maana kwani alihisi taarifa zake za kuzushiwa alihisi zimemfikia na hivyo hatoweza kumsaidia. Baada ya kupata matibabu na Mhisani wake Dereva Bodaboda kuruhusiwa katika Hospitali ya Chibumagwa, Chila alianza safari kwenda Chikuyu lakini si kwa Binamu yake.

Neema imekaribia.

Alitembea karibu umbali wa kilometa 10 akiwaza hili na lile bila majibu, alijiona ni mwenye mkosi na hakujua hatma yake, alikata tamaa na kuhisi kiu lakini kutokana ukweli kwamba likuwa porini ilimbidi kuvumilia na aliendelea na safari hadi alipotokeza katika Kijiji cha jirani na kuelekea nyumba moja kuomba maji. Alikariobishwa na Mzee wa makamo na aliyemkaribisha kwa bashasha Chila. Baada ya kusabahiana na kunywa maji Chila aliaga.

Lakini Mzee yule alimuomba Chila avute subira ili aongozane naye kwani naye alikuwa akielekea Chikuyu kama ambavyo yeye anaelekea huko, hivyo walifuatana na wakiwa njiani waliongea mengi ya Dunia, historia za maisha na masahibu ya Walimwengu, japo Chila hakuongea jambo lolote kumuhusu, lakini mzee yule alionesha kumuamini sana na alipendezwa na hekima za Chila na busara zake kama kijana kupitia maongezi yake yasiyo na papara.

Ama kweli giza likizidi neema imekaribia, kwani mara baada ya kufika Chikuyu Mzee yule alimuambia Chila watafute eneo kwanza wakae wazungumze, Mzee alimuelekeza mengi Chila na kumkabidhi jiwe dogo la Dhahabu akimuambia kilichomfikisha pale ni kutafuta usafiri kumfikisha Dodoma, ili akapate kuuza jiwe hilo apate peza za kulimia kwani msimu wa kilimo uliwadia.

Uaminifu ni hazina.

Mzee alidai hajui thamani halisi ya jiwe lile lakini aliona kwa busara za Chila anaweza kumsaidia kama kijana na haoni ulazima wa yeye kwenda Dodoma hali kijana yupo, akimsihi na kumuomba amvunjie ratiba zake ili aende na arudi katika mji ule ule alioomba maji na atampa kiasi cha fedha za mauzo kama shukrani.

Chila alikubali bila hiyana na ukizingatia hakuwa na pa kwenda hivyo aliona ni safari moja itakayomuanzishia nyingine, huku akijiwazia kuwa kiasi atakachopata kama malipo pia kitamsaidia kuanza upya maisha eneo jingine kwani hakuwa na eneo rasmi la kwenda, akajisemea moyoni “wema ni akiba” hivyo alifanikisha kila kitu kama alivyotaka mzee yule na aliporejea aliwasilisha fedha kwa Mzee yule ambaye alifurahi kwa uaminifu wa Chila na kuahidi kumtumia katika biashara zake hizo.

Kuanzia hapo maisha ya Chila yalibadilika, kwani alihusishwa kama mkuu wa usimamizi wa mashamba na uanzishaji wa miradi mingine ya kiuchumi kiasi wakapata mafanikio kwa haraka na mzee yule alijivunia kumpata kijana mwenye hekima na msimamizi wa miradi bila udanyanyifu, hivyo walipiga hatua kubwa kiasi cha kumiliki mashine nyingi za kukoboa mpunga, kusaga mahindi na walijenga maghala ya kuhifadhia mazao, nyumba za kuishi na biashara nk. hapo uchumi wa Chila uliimarika na akawa gumzo watu hawakuamini macho yao.

Changamoto ni kama kuweka ndimu kwenye supu.

Hakika kuna mengi ya kuongea na kusimulia, lakini tunachojifunza hapa ni kwamba, katika maisha yetu ya kila siku bila kutumia akili ipasavyo hatuwezi kuuona umuhimu wa changamoto. Na kama maisha yako ya kila siku hayana changamoto, basi ujue wewe ni mfu. Kumbuka unapopitia changamoto kwenye maisha ya kila siku inakupasa kuwa na imani kuu ya kumshukuru MUNGU. Chila alipitia changamoto nyingi na uvumulivu wake ulimfikisha nchi ya ahadi.

Kuna andiko aliwahi andika Kaka yangu John Mtangoo (Mkongwe katika Muziki na Mwimbaji wa Nyimbo za Injili) akisema, “Katika maisha usiziangalie Changamoto, angalia faida iliyoko mbele ya changamoto, zingatia furaha utakayoipata baada ya changamoto. Changamoto ni kama kuweka ndimu kwenye supu.” mapambano yaendelee.

@ wasalaam …. Humphrey Edward

Xavi aombwa kubaki FC Barcelona
Dabo aitafutia dawa Namungo FC