Beki wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans, Dickson Job amesema wanaifahamu vizuri Mamelodi Sundowns na wapo tayari kwa ajili ya kuvaana nao keshokutwa Jumamosi (Machi 30).
Young Africans itacheza na Mamelodi kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua va Robo Fainali, mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es salaam, Jumamosi saa 3:00 usiku.
Job ambaye ni Nahodha Msaidizi wa timu hiyo amesema wanafahamu ubora wa Mamelodi, lakini kwao wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanakabiliana nao ndani ya uwanja.
“Mazoezi tunayofanya yatakwenda kutoa picha halisi tutawezaje kushinda na kuwazuia wapinzani wetu, kwa kutumia ubora wetu na kikosi kipana tulichonacho, tumevuka hatua ngumu nyingi na kushinda sehemu ambayo wengi hawakutupa nafasi.”
“Jambo zuri tuna kocha anayeijua Mamelodi na ni lazima atatupa mbinu ya kuwamaliza, kwani anawafahamu vizuri, kwa kweli hatutacheza kwa hofu ya kuangalia jina la mchezaji au nchi kwani tunachotafuta ni ushindi utakaotupa wepesi wa kutinga Nusu Fainali, tunaamini tuna uwezo mkubwa wa kushinda mechi hii,” amesema Job.
Kocha wa kikosi hicho, Miguel Gamondi aliifundisha Mamelodi mwaka 2005/06 takribani miaka 18 iliyopita, hivyo ni wazi hata kikosi hicho kitakuwa na mabadiliko makubwa ukilinganisha na wakati huo.
Pamoja na Job kusema hivyo, lakini Mamelodi imeonekana kuwa na kasi kubwa ya kushambulia kwenye michezo yake ya hivi karibuni wakiwa wanapata mabao yao mengi dakika 45 za kwanza.
Katika mabao saba ambayo timu hiyo imefunga kwenye makundi, matano imefunga dakika 45 za kwanza huku ikifunga mawili tu kipindi cha pili cha mchezo.
Kwa upande wa Young Africans, imekuwa bora kipindi cha pili baada ya kufunga mabao sita kipindi hicho na matatu tu kati ya tisa ya jumla iliyonayo ikifunga kipindi cha kwanza.