Wakati Young Africans wakiendelea na maandalizi tayari kwa kukutana na Mamelodi Sundowns, Kocha Mkuu wa Mabingwa hao wa Afrika Kusini Rulani Mokwena amesisitiza kwamba wanatakiwa kuchukua tahadhari juu ya mchezo huo, kutokana na mabadiliko makubwa ya kiuchezaji ndani ya kikosi hicho.

Mokwena ameongeza kuwa ubora wa wachezaji wa Young Africans na wale wa Mamelodi utakuwa na nguvu kubwa ya kuamua mchezo huo utakaopigwa Jumamosi (Machi 30), Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 3:00 usiku.

Mokwena amesema timu yake inajiandaa kupata ushindi mbele ya Young Africans, lakini tahadhari yao nyingine ukiacha mastaa wenye uzoefu ni uwepo wa kocha Miguel Gamondi ambaye anajua karibu falsafa nzima ya klabu yao kwa kuwa aliwahi kufanya kazi hapo.

“Tunahitaji kushinda, tunajipanga kufanya hivyo hatutaangalia ukubwa wa jina letu tunataka ubora uamue mchezo. Haitakuwa mechi rahisi kwa pande zote. Tunawaheshimu Young Africans wako chini ya kocha anayeijua Mamelodi Gamondi ni kocha mkubwa,’ amesema Mokwena.

“Sisi tunajipanga kukutana na Young Africans bila kuangalia kuna mchezaji gani hayupo au yupo tunajiandaa kukutana na Young Africans iliyo kamili na kwa ubora wao.”

Wakati Mokwena akiyasema hayo mchambuzi maarufu wa soka kutoka Ivory Coast, Mamadou Gaye amewaonya Mamelodi kutowafuata Young Africans kwa mazoea kwani wanaweza kujikuta wanashangazwa.

Gaye akizungumza kwenye kipindi cha Pith Side kinachoendeshwa na Mamelodi, amesema Young Africans ina timu bora ambapo mchezo huo hautakuwa rahisi kutokana na muamko wa mashabiki wa timu hiyo.

“Msiwafuate Young Africans kwa mazoea watawashangaza itakuwa mechi ngumu kweli, Young Africans wanaona kama walicheza fainali ya Kombe la Shirikisho kwa nini sasa wasicheze Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kwa hiyo watajituma kutafuta ushindi,” amesema Gaye kwenye kipindi hicho.

“Kwanza mnatakiwa kutambua ule Uwanja wa Benjamin Mkapa unachukua mashabiki elfu sitini lakini siku hiyo watakaoingia ni elfu themanini na Young Africans ina mashabiki vichaa wanaojua kuipenda timu yao wako tayari kusafiri umbali mrefu kuifuata timu yao.”

“Wakati wanaifuata El Merreikh kule Rwanda walisafiri elfu mbili kuifuata timu yao na ikashinda huko huko kwa hiyo mjiandae msishangae hata mkipoteza kule Tanzania watakuja na huku Afrika Kusini.”

Mamadou ameongeza kwamba Young Africans ikiwa chini ya Gamondi, Kocha huyo anayeijua vyema Mamelodi ataingia kwenye mchezo kuendeleza msako wake wa kulitwaa taji la Afrika.

Sebo, Amoah wampa jeuri Dabo
De Jong kuendelea kukipiga FC Barcelona