Shirika la Kimataifa la kutetea haki za Binadamu la Amnesty International, limesema pande hasimu nchini Sudan zinazidi kutekeleza ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo kuwabaka wanawake, kuwaua raia kwa misingi ya kikabila, uporaji wa mali na kuharibu miundombinu ya mawasiliano.
Kupitia kwa mtafiti wake aliyepo Nchini Sudan, Abdulahi Hassan Amnesty inataka jamii ya kimataifa kuwajibisha wanaohusika katika mzozo wa Taifa hilo, wakati huu ambapo Ufaransa ikijitayarisha kwa kongamano la kujadili suluhu kwa mzozo wa Sudan, hapo April 15, 2024.
Zaidi ya watu 14,000 wameuawa nchini Sudan tangu kuanza mapigano hayo Aprili 15, 2023 ikiwa ni vita vya kugombania madaraka kati ya majenerali wawili walionyakua mamlaka katika mapinduzi ya mwaka 2021, Mkuu wa Jeshi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, na Makamu wake, Mohamed Hamdan Daglo, Kamanda anayeongoza kikosi cha RSF
Mapigano hayo yalizua malalamiko ya Kimataifa na wasiwasi wa kikanda, ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa mpaka na majirani wa nchi za Misri na Chad.