Mshambuliaji wa FC Barcelona, Robert Lewandowski, amekataa mkataba mnono nchini Saudi Arabia ili kubakia klabuni hapo, kwa mujibu wa ripoti kutoka Hispania.
Mchezaji huyo wa Kimataifa wa Poland alijiunga na Barca katika dirisha la usajili la kiangazi la 2022 na akaiwezesha klabu hiyo kutwaa taji lao la kwanza la La Liga katika kipindi cha miaka minne katika msimu wake wa kwanza, akifunga mabao 23 kwenye ligi na 33 katika mashindano yote.
Msimu wa pili wa Lewandowski katika klabu hiyo haukuwa na mafanikio mbele ya lango, huku Mshambuliaji huyo akistahimili hali duni ambapo alifunga mabao mawili pekee katika mechi 11 kabla ya mwaka mpya kuanza.
Kutokana na hali hiyo mbaya, uvumi ulianza kuzunguka mustakabali wa muda mrefu wa mshambuliaji huyo huko Barcelona.
Lewandowski amekuwa akihusishwa mara kwa mara kuhamia Saudi Arabia ili kuungana na nyota wenzake wakongwe, Karim Benzema na Cristiano Ronaldo, na imeripotiwa kwamba alipokea ofa ambayo itaongeza mara tatu’ mshahara wake anaoalipwa kwa sasa Barca, ili kuhamia Mashariki ya Kati.
Licha ya ofa hiyo nono, ripoti hiyo inaeleza zaidi kwamba Lewandowski ameamua kukataa ili kuona mwaka wa tatu na wa mwisho wa mkataba wake wa sasa pale Barcelona.
Mshambuliaji huyo amedokeza nia yake ya kubakia Barca kwa kusisitiza kwamba anatamani kucheza tena Camp Nou huku Uwanja huo ukifanyiwa ukarabati mkubwa.
“Ni moja ya malengo, kucheza tena Camp Nou,” amesema Lewandowski.
“Ni Uwanja mzuri bila shaka tunapaswa kusubiri miezi kumi nadhani. Katika msimu mpya, karibu mwisho wa mwaka, tutakuwa Uwanjani na tutaweza kucheza na watu wetu wote na mazingira hayo.
“Ninajisikia vizuri sana mjini, familia yangu pia, nina furaha na furaha sana. Nina furaha katika klabu, lakini pia katika kila kitu kingine.”