Cormac McCarthy alikuwa ni mwandishi wa Kiamerika ambaye aliandika riwaya kumi na mbili, tamthilia mbili, tamthilia tano za Luninga, na hadithi fupi tatu. Kazi zake mara nyingi zilijumuisha matukio ya mashambulizi na mtindo wake wa kuandika ulikuwa na sifa ya matumizi machache ya alama za maelezo.
Hata hivyo, inasemekakana Cormac McCarthy alikuwa hataki kufanya kazi nyingine za kujitafutia riziki zaidi ya uandishi kiasi cha kufanya yeye na wake zake kuishi katika shida na umasikini.
Kuna wakati wapekuzi wa mambo walitaka kujua kama jambo hilo ni kweli na ndipo walimfuata mmoja kati ya wakeze wa zamani kupata uthibitisho na alisema, “siku moja, kuna mtu alimpigia simu McCarthy, akimtaka kwenda Chuo Kikuu kuzungumzia vitabu vyake, kwa malipo ya $2000 (Tsh 4,500,00).”
“McCarthy aligoma na kumjibu kwamba kila kitu anachotakiwa kuzungumza kuhusu vitabu, kimo kwenye kurasa za vitabu vyake na baada ya hapo tuliendelea kuganga njaa wiki nyingine.”
McCarthy alizaliwa Providence, Rhode Island ingawa alilelewa huko Tennessee na mwaka 1951 alijiandikisha katika Chuo Kikuu cha Tennessee, lakini aliacha kisha kujiunga na Jeshi la Anga la Merika na alikuja kuyapata mafanikio yake katika uandishi na alifariki Juni 13, 2023, akiwa na umri wa miaka 89 huko Santa Fe.