Katika hali ambayo haikuzoeleka, Kocha Mkuu wa Coastal Union, David Ouma, ameanza mazoezi na kikosi chake kwa kuwaingia darasani badala ya uwanjani kama ilivyozoeleka.
Kocha huyo akiwa na kikosi chake na watu wake wa benchi la ufundi wameanza mazoezi ya darasani kwa ajili ya kuwafundisha vitu mbalimbali vya soka kinadharia ili wachezaji wapate kumsikiliza kwa makini wakiwa wametulia.
Klabu ya Coastal Union, imechapisha picha kwenye moja ya akaunti yake ya mtandao wa kijamii, ikionyesha kocha huyo akiwa bize amesimama mbele ya wachezaji akiwaeleza mambo mbalimbali wanayotakiwa kufanya wakiwa uwanjani, huku wachezaji wake wakiwa wamekaa kwenye viti na madawati kama wanafunzi, wakiwa na jezi za klabu hiyo na wakisikiliza kwa makini.
Kocha huyo amesema kuwa, mwalimu siku zote anatakiwa kufundisha kwa vitendo na kwa maneno pia, hivyo amewaingiza darasani kipindi hiki ambacho wametoka kwenye mapumziko, kabla ya kuingia gym, na hatimaye uwanjani.
“Siku zote mwalimu kazi yake ni kufundisha kwa mbinu zote, ili mradi ni kuhakikisha malengo yanatimia,” amesema Ouma
Ofisa Habari wa Coastal Union, Abbas El Sabri, amesema hiyo yote ni mipango ya viongozi na mwalimu, ambapo uongozi umempa kocha kila anachohitaji kuhakikisha malengo ya kumaliza ligi wakiwa nafasi ya nne na kucheza mechi za kimataifa msimu ujao yanafanikiwa.
“Hii ni mipango ya kuhakikisha kwanza tunaingia Robo Fainali ya Kombe la FA, na Ligi Kuu Tanzania Bara,” amesema El Sabri.