Rais mpya wa Senegal ni Bassirou Diomaye Faye, mwenye umri wa miaka 44, mzaliwa wa eneo la Ndiaganiao aliyefanikiwa kuingia madarakani baada ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa kiongozi wa upinzani, Ousmane Sonko ameapishwa rasmi kuliongoza Taifa hilo, huku Wasenegal wengi wakiwa na matumaini naye.
Alikuwa Naibu wa Sonko katika chama cha Pastef kabla ya chama hicho kufutwa na mamlaka. Faye amesomea maswala ya ukaguzi wa kodi na ametokea katika familia ya wakulima. Anajulikana kwa msimamo wake thabiti na ahadi yake ya kuongoza Senegal kwa kuzingatia sheria.
Marafiki wa karibu wa Bassirou Diomaye Faye wanamsifia kuwa ni mtu mwenye msimamo thabiti na asiyeepuka maamuzi magumu. Hii imemfanya kuwa ngome muhimu ndani ya chama cha Ousmane Sonko na sasa ndiye analiongoza taifa la Senegal.
Kinachoshangaza ni kwamba, miezi michache tu iliyopita, Faye alikuwa ameketi katika chumba cha magereza, akiwa hajulikani kwa kiasi fulani nje ya chama chake cha upinzani cha Pastef.
Kila kitu kilibadilika baada ya Ousmane Sonko, ambaye pia alizuiliwa gerezani kwa mashtaka ya uasi mwezi Julai na kuzuiwa kushiriki katika uchaguzi wa kumrithi Rais Macky Sall kumsafishia njia hadi kutoka gerezani, kuchukua kinyang’anyiro hicho na siku ya kutimiza miaka 44 – akaibuka mshindi baada ya mpinzani wake kukubali kushindwa.
Alikamatwa Aprili 2023, miezi michache kabla ya Sonko pia kushikiliwa na kushtakiwa kwa kudharau mahakama na kukashifu mahakimu, mashtaka ambayo Faye alikana. lakini tofauti na Sonko, yeye hakuzuiwa kushiriki katika uchaguzi.
Muungano wa vyama zaidi ya 100, na baadhi ya vigogo wa kisiasa akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Aminata Toure, vilijiunga na kampeni ya Faye chini ya bendera ya “Doimaye mooy Sonko”, ambayo kwa lugha ya kiwolofu ina maana ya “Diomaye ni Sonko.”
Kutokana na sheria ya jumla ya msamaha iliyopitishwa muda mfupi kabla ya kura ya kupunguza mivutano ya kisiasa, Sonko na Faye walitolewa gerezani huko Dakar, kisha wakaandamana na maelfu ya wafuasi ambao walicheza na kuimba usiku kucha wakipiga kampeni, kuzunguka nchi nzima na kuwavutia maelfu ya watu kwenye mikutano na misafara yao.
Faye hajawahi kuchaguliwa katika wadhifa wowote wa kisiasa hapo awali, na ushindi wake huu unamfanya awe rais mpya wa Senegal akiwa na ahadi ya kuongoza nchi hiyo kwa uwajibikaji, je? nini atafanya. Hili ni swali la kila mmoaj na muda utaongea.