Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi amesema amefurahishwa na kurejea kwa viungo Khalid Aucho na Pacome Zouzoua waliokosa mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, mwishoni mwa wiki na timu hizo kutoka sare ya bila kufungana.

Nyota hao walikuwa kwenye msafara wa watu 60 wa wachezaji, benchi la ufundi na viongozi waliotua salama Johannesburg, Afrika Kusini kwa mchezo wa marudiano keshokutwa Ijumaa (Aprili 05) Uwanja wa Versfeld jijini Pretoria.

Akizungumza baada ya kuwasili Afrika Kusini, Gamondi amesema kurejea kwa nyota hao kunaongeza hali ya kujamini na upana wa kikosi chake kuelekea mchezo huo muhimu ambao Young Africans watakuwa wanasaka kuingia Nusu Fainali yao ya kwanza kwenye historia ya michuano hiyo.

“Khalid Aucho na Pacome Zouzoua ni wachezaji wa daraja la juu na kurejea kwao kunaongeza hali ya kujiamini na upana wa kwenye kikosi changu. Hakuna asiyefahamu uwezo wa Aucho na Pacome kwenye timu ya Young Africans. Tumekuja Afrika Kusini tukiwa na lengo moja tu kukamilisha dakika 90 za marudiano kwa kuipeleka Young Africans Nusu Fainali,” amesema kocha huyo raia wa Argentina.

Amesema walicheza vizuri mhezo uliopita na kuwabana wapinzani wao kuingia kwenye eneo la hatari na kujikuta muda mwingi wakicheza kwenye eneo lao, na kuongeza wanajua nini wanatakiwa kufanya kwenye mchezo wa marudiano kutimiza malengo yao.

“Tumekuja kutafuta matokeo na kuhakikisha hatufanyi makosa yanayoweza kutugharimu, naamini tutakuwa vizuri zaidi kwenye mchezo huu, tunajua ubora wa Mamelodi na tunajua wakiwa kwao wanakuwa na nguvu kubwa, tunajipanga kwa yote,” ameongeza Gamondi.

Mratibu wa Young Africans, Hafidh Saleh amethibitisha wachezaji wote wakiwamo Pacome, Aucho na mlinzi Yao Koussi ni sehemu ya msafara wa watu 60 uliotua nchini Afrika Kusini.

Jana jioni, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana aliandika katika akaunti yake ya X: “Muda mchache uliopita nimewaongoza Diaspora wa Tanzania nchini Afrika Kusini kuipokea Timu ya YOUNG AFRICANS. Timu ina hamasa kubwa ya mchezO wao na MAMELODI SUNDOWNS FC tarehe 05 Aprili, 2024. Watanzania wote tuiombee ushindi na tuiombee pia ushindi Simba SC huko Cairo, Misri”.

Katika hatua nyingine, msafara wa mashabiki 48 wa Young Africans wanaokwenda Afrika Kusini kwa mabasi kuishangilia timu yao, wanaendelea na safari kupitia Zambia baadaye Zimbabwe kabla ya kuingia Afrika Kusini.

MAKALA: Faye amebeba tumaini jipya la Wasenegali