Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amelazimika kuwatuliza Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo, kufuatia kuhoji baadhi yao kusafiri kwa gharama zao wenyewe kwenda Cairo, Misri.

Simba SC imetoa taarifa za baadhi ya Mashabiki wa klabu hiyo kusafiri kwa gharama zao wenyewe, kwenye msafara wa klabu hiyo ambao tayari umeshawasili mjini Cairo, tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali dhidi ya Al Ahly.

Sintofahamu kwa Mashabiki na Wanachama wa Simba SC imeibuka kufuatia wenzao Young Africans kupewa msaada wa kusafirishwa bure na Serikali kuelekea Afrika Kusini, kwa ajili ya kuishangilia timu yao itakapokuwa uwanjani keshokutwa Ijumaa (Aprili 05), dhidi ya Mamelodi Sundowns.

Ahmed Ally ametuliza hali hiyo kwa kuandika ujumbe kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, huku akiahidi kuielezea kwa undani sintofahamu hiyo baada ya mchezo wao dhidi ya Al Ahly keshokutwa Ijumaa (Aprili 05).

Ahmed Ameandika: Baadhi ya Mashabiki wa Simba waliojilipia nauli zao kusafiri kwenda kuipa support timu yao Nchini Misri. Kila shabiki amejilipia Dola 1200 sawa na Milioni 3,126,000.

Hili swala la Serikali kusafirisha Mashabiki nitatoa maoni yangu nikimalizana na Al Ahly, Sasa hivi akili inawaza namna ya kufuzu Nusu Fainali, Ila msimamo wangu ni kwamba si jambo jema hata kidogo.

Kwa Mashabiki mpira ni starehe hivyo Serikali haiwezi kugharamia watu kwenda kustarehe.

Tena bora ingekua imetoa usafiri tu. Lakini wametoa Posho Dola 500 kila kichwa sawa na Milioni 1,200,000 kwa ufupi hawa Mashabiki wamenuniliwa na wanalipwa kuishangilia timu yao.

Na hao sio Mashabiki wa kawaida ni Machawa wanaotetea maslahi ya viongozi wao yaani Serikali imelipia Machawa wa watu.

Kuwalipia nauli sio kuwapenda ni kufuga tatizo ambalo baadae hatutaweza kulitatua.

Leo unalipia mashabiki wa klabu, kesho Ali Kiba ataiomba Serikali iwagharamie mashabiki wake kwenda Marekani kufanya show utamnyima??

Twaha Kiduku ataomba aende kupigana Uingereza na mashabiki wake utamnyima??

Halafu nyie Nyuma Mwiko acheni kuzuga huwezi kulipia nauli watu 48 ukajidai eti unawapenda mashabiki zenu, Wakati kwenye mechi yenu juzi Mashabiki wameumia, wamepigwa mabomu ya machozi, watu wamepata vilema, na hamjasema chochote halafu uje uzuge eti unawapenda watu wenu.

Ndugu zangu wana Simba hili swala lisiwatie unyonge na wala Serikali yetu haina nia ya kufanya ubaguzi.

Sisi tuendelee na utamaduni wetu kujisimamia tukipata msaada tutachukua lakini katu tusilemae kusubiri dezo.

We are Simba 💪 Sisi ni Wakubwa, Sisi ni Wafalme, Sisi tuna hadhi kubwa.

Lets focus na mechi yetu ya Ijumaa.

Taiwan: Tetemeko lauwa tisa, tahadhari ya Tsunani yatolewa