Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, Judith Nguli ametoa wito kwa Wananchi wa Wilaya hiyo kutumia fursa ya Maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani kuchunguza Afya bure pamoja na kushiriki katika mazoezi ili kujikinga na Magonjwa Yasiyoambukiza.
Nguli ameyasema hayo Ofisini kwake Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro mara baada ya kufanya Kikao na Timu kutoka Wizara ya Afya,Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya Mvomero ikiwa ni katika Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani April 7, 2024 yakiwa na kaulimbiu isemayo “Afya Yangu,Haki Yangu”.
Amesema, katika kuelekea Siku ya Afya Duniani April 7, 2024 ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa kuchunguza Afya zao kuanzia April, 4-7, 2024 ambapo pia kutashirikisha Michezo mbalimbali.
“Wananchi wa Mvomero tuchangamkie kuchunguza Afya Zetu katika kuelekea Siku ya Afya Duniani maana kutakuwa na Uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa Kizazi, Shinikizo la juu la damu, lishe hivyo nawakaribisha sana,” alisema.
Aidha, kupitia Maonesho hayo itakuwa ni fursa kubwa kwa Wananchi kufanya mazoezi kupitia Mashindano ya Michezo yatakayosaidia kuimarisha Afya ya mwili huku akiipongeza Wizara ya Afya kwa kuchagua Wilaya ya Mvomero kufanyiwa Maadhimisho hayo.