Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, limechangia kujenga uchumi imara kwa kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo wananchi kuwa na uhuru wa kufanya shughuli za uzalishaji mali bila hofu.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax, ameyasema hayo jijini Dodoma, wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema, “katika kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uhuru na usalama wa nchi, wizara kupitia JWTZ imechangia katika kujenga uchumi imara ambapo wananchi hujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali bila hofu.”

Dkt. Tax ameongeza kuwa, yote yamewezekana kutokana na kuwepo kwa sera, sheria, kanuni na mipango madhubuti katika ulinzi wa nchi, vinavyotoa fursa kwa wananchi kujikita katika ujenzi wa taifa lao.

Aidha, amesema Serikali kupitia wizara hiyo imeendelea kutekeleza, na kuliimarisha jeshi kwa kulipatia zana na vifaa bora na vya kisasa, rasilimali watu, na nyenzo za kufanyia mazoezi ili kuwa imara wakati wote.

“Mafanikio mengine ni ushiriki wa wizara kupitia taasisi zake, hususan JWTZ katika kukabiliana na majanga au maafa mbalimbali pale yanapotokea. Katika kutekeleza jukumu hilo, JWTZ imeendelea kushiriki kikamilifu katika kutoa misaada ya uokoaji na ile ya kibinadamu kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa,” amesema.

Waziri Mkuu: Mapato ya ndani yafikia Trilioni 17
Siku ya Afya Duniani: Tuchunguze afya zetu - DC Nguli