Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kati ya Julai, 2023 na Januari, 2024 Serikali imefanikiwa kukusanya sh. trilioni 17.1 ambazo ni sawa na asilimia 95.9 ya lengo la kukusanya sh. trilioni 17.9.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Aprili 3, 2024), wakati akiwasilisha Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2023/2024 na Mwelekeo wa Kazi zake kwa mwaka 2024/2025 Bungeni, jijini Dodoma.

“Katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Januari, 2024 mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia shilingi bilioni 17,188.4, sawa na asilimia 95.9 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 17,929.8 na ukuaji wa asilimia 10.0 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2022/2023.”

Amesema kati ya mapato hayo, sh. bilioni 15,159.8, sawa na asilimia 97.9 ya lengo la kukusanya sh. bilioni 15,492.7 zilikusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huku Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Serikali zikikusanya sh. bilioni 1,374.5, sawa na asilimia 78.2 ya lengo la kukusanya sh. bilioni 1,758.3. “Mapato yaliyokusanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia sh. bilioni 654.1 ikiwa ni asilimia 96.4 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 678.8.”

Amewataka wafanyabiashara wote wahakikishe wanatoa risiti halali za kielektroniki za mauzo ya bidhaa na huduma wanazotoa. “Vilevile, niwakumbushe wananchi wote kudai risiti halali za kieletroniki kila wanapofanya ununuzi wa bidhaa na huduma ili kudhibiti upotevu wa mapato na hivyo kuimarisha uwezo wa Serikali katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi ikiwemo maji, elimu na afya.”

Aidha ameongeza kuwa, katika mwaka 2024/2025, Serikali itaendelea kuweka vipaumbele zaidi kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa bajeti kwa kuimarisha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kuwianisha, kufuta au kupunguza viwango vya kodi, tozo na ada zinazoonekana kuwa kero.

Ujenzi SGR umetumia Trilioni 10.69 - Serikali
Dkt. Tax: Uhuru, Usalama wa Nchi umeimarisha Uchumi