Uongozi wa Coastal Union umesema haujamwekea mtego wowote Kocha Mkuu wa timu hiyo raia wa Kenya, David Ouma, ikiwamo wa kupoteza mechi ili kumfuta kazi ya kukinoa kikosi hicho.
Kauli hiyo imekuja baada ya taarifa kuzagaa kuwa viongozi hao wamempa mechi moja na kama akipoteza anafungashiwa virago vyake huku akitajwa aliyekuwa Kocha wa Tabora United, Goran Kopunovic, anatarajiwa kubeba mikoba yake.
Ofisa Habari wa Coastal Union, Abass Elsabri, amesema hakuna ukweli wowote juu ya kutaka kumuondoka wala kumpa mtihani wa kushinda baadhi ya mechi.
Amesema ataendelea kukinoa kikosi cha timu hiyo kulingana na mkataba wake wa miaka miwili utakapafikia tamati kwa sababu amefanikiwa kuitoa timu kutoka nafasi ya 14 hadi 4.
“Hayo mambo yanatengeneza kutuondoa katika mstari kwa sababu kuna taarifa kuwa baadhi ya wachezaji wetu kuhusishwa na klabu kongwe hapa nchini, lakini pia kuna hilo jambo la kocha Ouma kuachana naye.”
“Mashabiki wetu wanatakiwa kupuuza hizo tetesi na kushikamana kuwa wamoja, hakuna ukweli juu ya kutaka kumfukuza kocha wetu wala kumpangia mechi kuwa asiposhinda tutamuonda hilo halipo,” amesema Abass
Ameongeza kuwa kwa sasa akili na nguvu zao wanazielekeza katika michezo iliyopo mbele yao ili kushinda na hatimaye kubaki kwenye nafasi ya juu.
Coastal Union inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na alama 30, wakishinda nane, sare sita na kupoteza michezo saba na sasa imefuzu kucheza Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRBD.