Mkoa wa Tanga hii leo Aprili 9, 2024 unatarajia kuupokea Mwenge wa Uhuru ukitokea Mkoani Kilimanjaro ambapo utazinduaa miradi yenye thamani ya zaidi ya bilioni 40 na utakimbizwa kwenye Halmashauri 11 za mkoa wa Tanga, ukiendelea kuhamasisha na kuwaelimisha wananchi juu ya mapambano dhidi ya Rushwa, Malaria, VVU /UKIMWI, Dawa za Kulevya na uzingatiaji wa Lishe bora.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amesema mapokezi ya Mwenge huo yatafanyika katika Kijiji cha Mazinde kilichopo Wilayani Korogwe ambapo utakagua na kuweka mawe ya msingi miradi 87.
Amesema, Mwenge pia unatarajiwa kukimbizwa umbali wa kilomita 1635 na na baada ya kupitia miradi na kuikaagua na baada ya kumaliza mbio zake utakabidhiwa Mkoani Morogoro.
“Ujumbe maalumu wa Mwenge kwa mwaka 2024 ni tunza mazingira na shiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa endelevu kwa hiyo tunategemea kwenye miradi ya mwenge kutakuwa na utunzaji wa mazingira ,kutakuwa na kutakuwa na ujumbe wa kupiga vita Dawa za Kulevya,” alisema Batilda.
Hata hivyo aliwataka Wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kuupokea na kuulaki Mwenge katika mapokezi, barabarani, kwenye miradi na maeneo ya mikesha.