Katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano, Jeshi la Polisi Nchini limefanikiwa kupeleka Polisi kata 2,608 wenye cheo cha Mkaguzi na Mkaguzi Msaidizi, kwenye kata zote za Tanzania Bara.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya ndani, Mhandisi Hamad Masauni wakati akizungumza na Waandishi wa Habari na kuongeza kuwa pia wapo Askari wa vyeo mbalimbali 1,353 ambao wamepangwa kwenye shehia.
Amesema, “na kwa upande wa Zanzibar wakaguzi 169 na Askari wa vyeo mbalimbali 134 nao wamepangwa kwenye shehia, zipo faida mbalimbali ambazo serikali imezipata tangu kuanza kwa kutekelezwa kwa falsafa ya Polisi jamii moja wapo ikiwa imesaidia kubuni miradi mbalimbali ya kuzuia na kubaini uhalifu.”
Masauni amebainisha kuwa, Serikali imepata faida ya kujenga ubia endelevu wa ushirikiano baina ya Jeshi la Wananchi katika kubaini na kuzuia uhalifu, hali ambayo imesaidia kutatua changamoto za kijamii kabla madhara hayajatokea katika jamii.
“Kupitia Polisi Jamii, Polisi kata wamesaidia kuwajengea uelewa Wananchi katika eneo la uwezo wa kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu unaojitokeza na Jeshi la Polisi limefanikiwa kuanzisha vyuo vipya vya Polisi vitatu ukilinganisha na vyuo viwili ambavyo vilikuwepo kabla ya Muungano,” amesema Masauni.
Aliongeza kuwa, “Vyuo hivyo ni Chuo cha Polisi Zanzibar, Chuo cha Polisi Kidatu na Chuo cha Polisi Wanamaji Mwanza, ambavyo vinalenga kuwajengea uwezo Askari wa kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu Nchini, Vyuo vya zamani ni Chuo cha Taaluma ya Polisi, Dar es salaam ambacho tumekirithi na kimeendelea kuboreshwa.”
Kuhusu Idara ya Uhamiaji, amesema imeanza kutumia mfano wa uhamiaji mtandao unaounganisha mifumo yote ya utoaji huduma za kiuhamiaji kama vile paspoti, visa, vibali vya ukaaji pamoja na udhibiti na usimamizi wa mipaka kwa njia ya kielektroniki.