Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amepokea msaada wa mchele, Maharage na unga tani 300 kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ukiwa ni mchango wake binafsi kwa ajili ya waathirika wa mafuriko yaliyotokea katika Mto Rufiji kwa Wilaya za Rufiji na Kibiti uliowasilishwa na Innocent Mbilinyi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Ikwiriri Wilayani Rufiji Mkoani Pwani wakati wa kupokea msaada huo, Kunenge ameshukuru kwa misaada huo ambapo tayari tani 32 za mchele zimekwisha wasili na kupokelewa, huku tani zingine zikiwa Barabarani kuletwa Wilayani humo.

Kunenge amesema Rais Samia amekuwa akiwapelekea misaada mingi ya aina mbalimbali kwa ajili ya Wananchi wa Mkoa huo wanapopatwa na maafa mbalimbali kutoka Serikalini, lakini kwa safari hii msaada huo wa tani 300 ni ameuoutoa katika mfuko binafsi.

“Mheshimiwa Rais amekuwa akituletea misaada mingi kutoka serikalini lakini msaada huu ametoa yeye binafsi na sisi tunaahidi tutaigawa misaada hii kwa kusimamia vizuri kwa walengwa kama ambavyo yeye imempendeza kutoa msaada huu,” alisema Kunenge.

Aidha, aliongeza kuwa, “lakini pia nimshukuru Mbunge wa jimbo la Rufiji na Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa kwa kazi kubwa anayoifanya ya kututafutia misaada mbalimbali na sisi tumuahidi kwamba misaada yote inayokuja tutaisimamia vizuri kwa kutumiwa na walengwa kama ilivyokusudiwa.”

Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Innocent Mbilinyi amesema msaada huo wa Mchele daraja la kwanza ni tani 100, Maharage tani 100 na Unga tani 100 ambapo tani zilizofika ni tani 32 wakati tani zingine zikiendelea kuja ambapo Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele ataratibu usambazaji kwa walengwa katika Wilaya za Kibiti na Rufiji.

Serikali yapanga kuondoa changamoto sekta ya ajira
Masauni abainisha mafanikio ya Jeshi la Polisi