Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, imepanga kuondoa changamoto zinazowakabili waombaji wa fursa za ajira nchini, kwa kuendesha usaili wa kuandika/mchujo Kidijitali wenye lengo la kuwafikia waombaji wote mahali walipo Tanzania bara na Zanzibar.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma,George Simbachawene ameyabainisha hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari na kusema ili kukabiliana na changamoto zilizokuwepo, wamesanifu na kujenga mfumo wa kufanya usaili kwa njia ya kielektroni (Online Aptitude Test System), – OATS na uliokamilika kwa asilimia 98.
Amesema, “mfumo huu utawezesha wasailiwa kufanya usaili wa kuandika/mchujo kwa njia ya kidijitali katika eneo la karibu na mahali anapoishi, kutumia muda mfupi, kuepuka gharama za usafiri, malazi na changamoto za ajali, kwa hatua za mwanzo, usaili huu utafanyika katika vituo maalum.”
“Utafanyika pia katika taasisi za Umma na binafsi, vituo hivi ni pamoja na Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA), Vyuo Vikuu vya Umma na binafsi, Baadhi ya vyuo vya kati vya umma na binafsi, Vyuo vya Ualimu na baadhi ya Sekondari zenye miundombinu ya Maabara ya Kompyuta zilizounganishwa na huduma ya intaneti,”amesema Simbachawene.
Aidha, ameongeza kuwa pia Serikali imekuza uchumi wa Kaya Maskini kwa kuhamasisha Walengwa kuunda vikundi vya kuweka akiba, kukopeshana na kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji mali ili kuinua kipato cha Kaya.
Amesema, “Tanzania Bara vikundi vya kuweka akiba 26,842 vyenye wanachama 358,846 viliundwa katika Mamlaka za Maeneo ya utekelezaji na viliweza kuweka akiba ya kiasi cha Shilingi bilioni 6.3, kati ya fedha hizo kiasi cha bilioni 2.7 kilitolewa kama mikopo kwa wanachama wake.”
“Kwa upande wa Unguja na Pemba, jumla ya vikundi 3,211 vyenye wanachama 45,948 vimeundwa na vimeweza kukusanya jumla ya akiba ya shilingi bilioni 1.6 kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 365.9 kilikopeshwa kwa wanachama,” aliongeza Simbachawene.
Hadi kufikia Machi, 2024, walengwa wamepewa mafunzo ya stadi za msingi za kuendesha shughuli za kiuchumi kwa pande zote za Muungano ikiwa Tanzania Bara walengwa 27,964 kutoka Halmashauri 33 waliopatiwa mafunzo na Ruzuku ya Uzalishaji ya kiasi cha Shilingi bilioni 8.6.