Mashabiki na Wanachama wa Young Africans wameombwa kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa wingi Jumamosi (Aprili 20), kwa ajili ya kuipa nguvu timu yao itakapokuwa kwenye heka heka za kuwania alama tatu dhidi ya Simba SC.

Young Africans wanakwenda kwenye mchezo huo wakiwa na hamasa kubwa ya kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo, wakiiacha Simba SC kwa tofauti ya alama tisa.

Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe amesema Mashabiki na Wanachama wao wana umuhimu mkubwa katika mchezo huo, hivyo wanapaswa kufika Uwanjani kwa wingi.

Amewataka Mashabiki na Wanachama wa Young Africans, kujitokeza Uwanjani na kuifanya Kariakoo Derby kuwa kama Kilele cha Siku ya Wananchi kwa kujaza uwanja na kutowapa nafasi ya wapinzani wao kuwa wengi.

“Asitokee Mwanayanga akabaki nyumbani na baada ya matokeo akajisifia, tunahitaji siku hiyo kuwa ni Kilele cha Siku ya Wananchi na tusiwape nafasi mashabiki wa upande wa pili kuwa wengi,” amesema Kamwe

Hata hivyo Kamwe amewaomba Mashabiki na Wanachama wao kuachana na fikra ya kuwa mpinzani wao amechoka na hajapata matokeo mazuri, bali wanatakiwa kufikiria namna ya kuzipata pointi tatu mbele ya Simba SC.

Amesema mechi ya Simba SC na Young Africans ina umuhimu wake, na kwamba haitakiwi kwenda uwanjani na mawazo ya pointi tatu kwa kufikiri mpinzania wao amechoka, jambo ambalo wanatakiwa kuliondoa kichwani na kutambua wanaenda kukutana na timu tishio.

“Hatuitazamani Simba SC kama wanavyoitazama mashabiki, bali kwetu ni timu tishio na tuko nao katika vita, kwa sababu wana wachezaji wazoefu kwenye kucheza Derby kubwa na tofauti pia viongozi makini na wenye mipango na ubora wa hizi mechi,” amesema Kamwe.

Kuhusu majeruhi, amesema baadhi ya wachezaji wamerejea akiwamo Kennedy Musonda na Pacome Zouzoua yuko katika hatua nzuri ya kurejea katika hali yake ya kwaida.

“Hatuwezi kuwalazimisha wachezaji kucheza kwa sababu Young Africans ina kikosi kipana na tunaenda siku hiyo kwa roho ya kikatili,” amesema Kamwe

Shughuli za uokozi: Ulega amkabidhi Boti Kunenge
Serikali yapanga kuondoa changamoto sekta ya ajira