Wakati Simba SC ikijiandaa na mchezo wa Kariakoo Dabi, Uongozi wa Klabu hiyo umewataka Mashabiki na Wanchama kuendelea kukiamini kikosi chao, huku ukiwataka kujitokeza Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumamosi (Aprili 20).

Simba SC itakuwa mgeni wa mchezo huo, huku ikikumbuka kupoteza mchezo wa Mzunguuko wa kwanza kwa kuambulia kisago cha mabao 5-0, kutoka kwa Watani zao wa Jadi Young Africans Novemba mwaka 2023.

Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba SC Ahmed Ally amesema Wanachama na Mashabiki wa Klabu hiyo wanapaswa kuwa kitu kimoja kuelekea katika mchezo huo, huku akiamini hakuna kitakachoshindikana.

Amesema nguvu ya pamoja kutoka kwa watu wa Simba SC ndio silaha kubwa itakayowawezesha kupambana na kupata matokeo mazuri dhidi ya Young Africans Jumamosi (Aprili 20), hivyo hawana sababu ya kufungwa kwa mara ya pili katika msimu mmoja.

“Tulipoteza duru ya kwanza, hatupo tayari kuona tunapoteza tena kwa mara ya pili kwenye msimu mmoja. Niwaombe Wanasimba ambao wamekata tamaa, mioyo inavuja damu, waje uwanjani kuipigania Simba SC na kurejesha heshima yetu, tukishikamana hakuna wa kutuzidi nguvu, ajenda yetu ni kwenda kumfunga mtani,”

“Malengo yetu sasa ni mechi ya Jumamosi dhidi ya Young Africans, ni mechi inayobeba taswira ya soka la Tanzania ambao unabeba heshima ya Tanzania na sisi kama Simba SC tunayo nafasi ya kwenda kuweka heshima yetu kwenye mchezo wa dabi. Ni lazima tuhakikishe tunaingia vizuri na kushinda.” amesema Ahmed Ally

Wakati huo huo kikosi cha Simba SC kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam leo Jumanne (Aprili 16) kuelekea visiwani Zanzibar kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Young Africans.

Kikosi cha Simba SC jana Jumatatu (Aprili 15) kilianza mazoezi katika Uwanja wa Mo Simba Arena, Bunju jijini Dar es salaam, baada ya kurejea kutoka mkoani Singida kilipocheza mchezo dhidi ya Ihefu FC, Jumamosi (Aprili 13) na kuambulia sare ya 1-1.

Polisi Kagera wachunguza tukio la mauaji ya Mwanafunzi
PPRA, PRAZ wabadilishana uzoefu mifumo ya ununuzi