Mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa na Klabu ya Manchester United ya England Anthony Martial, huenda akapata nafasi ya kufufua makali yake, endapo atafanikiwa kuondoka Old Trafford.
Martial amekuwa na wakati mgumu wa kutumika kwenye kikosi cha kwanza cha Manchester United, majeraha ya mara kwa mara, hali ambayo inamnyima nafasi ya kurejea katika kiwango chake kama alichotua nacho klabuni hapo mwaka 2015.
Mabingwa wa zamani wa Italia Juventus wanatajwa kuwa kwenye mpango wa kumsajili Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 mwishoni mwa msimu huu, na inaaminiwa endapo dili hilo litakamilishwa basi Martial atapata nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Mkataba wa sasa wa Martial utafikia tamati mwishoni mwa msimu huu 2023/24, na dili lake kuondoka Old Trafford litainufaisha Juventus, kwani itampata kama mchezaji huru.
Mtandao wa Tuttosport umeeleza kuwa mabosi wa Juventus wameshawishiwa kumsajili Mshambuliaji huyo, huku Benchi la Ufundi la Juventus likiamini ataweza kuwasaidia katika harakati zao za kurejesha Ufalme wa soka nchini Italia kuanzia msimu ujao.
Hata hivyo Martial anatajwa pia kuwaniwa na klabu ya Tottenham inayonolewa na Kocha Mkuu kutoka nchini Australia Ange Postecoglou.
Hata hivyo klabu hiyo yenye maskani yake makuu kaskazini mwa jijini London, huenda ikazidiwa ujanja na Juventus, inayopewa nafasi kubwa kumsajili Mshambuliaji huyo.