Kocha Mkuu wa Arsenal Mikel Arteta amefanya mawasiliano na beki wa zamani wa Manchester United, Gabriel Heinze kwa lengo la kumtaka nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Argentina kuwa msaidizi wake msimu ujao.
Arsenal wanasaka mbadala wa kocha wa kumsaidia Arteta baada ya Albert Stuivenberg na Carlos Cuesta waliokuwa wanaifanya kazi hiyo wote wakitajwa kutakiwa kuwa makocha wakuu kwenye klabu nyingine.
Arteta alipewa kazi ya kuwa kocha mkuu wa Arsenal baada ya kuwa msaidizi wa Pep Guardiola kwenye klabu ya Manchester City na sasa anataka kumpa kazi ya kumsaidia mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United.
Kiwango kinachooneshwa na Arsenal msimu huu kimeshuhudia makocha wa klabu mbalimbali Barani Ulaya wakiwania huduma za wasaidizi wa Arteta wakati huu Washika Bunduki hao wakipambana kushinda taji la Ligi Kuu ya England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kiungo huyo wa zamani wa Paris Saint-Germain na Glasgow Rangers anataka kumfanya Heinze kuwa msaidizi wake sambamba na majina mengine yanayotakiwa na Mhispania huyo.
Heinze aliitumikia Manchester United chini ya Alex Ferguson mechi 83 kati ya mwaka 2004 na 2007 kabla ya kuondoka kwenye klabu hiyo kwa sababu ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Msimu wake wa kwanza kwenye klabu hiyo inayotumia Uwanja wa Old Trafford akishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa klabu hiyo kabla ya kuumia na beki wa kushoto wa kimataifa wa Ufaransa Patrice Evra kuchukua nafasi yake na baadae Heinze akauzwa Real Madrid.
Beki huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 45, amekuwa akifundisha klabu mbalimbali Marekani ya Kusini na Marekani tangu atundike daluga miaka 10 iliyopita na sasa anafanya mazungumzo na Arteta kuungana naye kwenye kikosi cha Arsenal.
Arteta na Heinze walicheza pamoja mwanzoni mwa maisha yao ya soka kwenye klabu ya PSG ya Ufaransa.