Eva Godwin – Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi amesema Serikali inaendelea na Mipango yake ya kupanga mikakati ya namna ya kupambana na ugonjwa wa Malaria na Mbu wanaoeneza Ugonjwa huo.

Akizungumza katika kikao cha ngazi ya Makatibu Wakuu wa Wizara kilichohusu ushirikiano wa Kisekta jijini Dodoma, Dkt. Yonazi alisema lengo ni kuhakikisha Serikali inatengeneza mfumo mzuri wa namna ya kupambana na malaria nchini, ili kuokoa nguvu kazi ya Taifa na rasilimali zitakazotumika katika kutibu ugongwa huo.

Amesema, “tunaamini kwamba tunapokuwa na Taifa ambalo halina Malaria tunaweza kuongeza Tija katika uchumi na katika maendeleo kwa haraka katika Nchi yetu kwa hivyo nitoe wito kwa Makatibu Wakuu na wadau wote tunaoshirikiana kuhakikisha kwamba tunaongeza nguvu ili tuweze kupambana na ugonjwa wa Malaria na vilevile mbu waenezao ugonjwa huo.”

Aidha Katibu Mkuu Yonazi Alitoa wito kwa Jamii ya Watanzania kuendelea kushirikiana na Serikali na Wadau mbalimbali, ili kuhakikisha, jamii zinapambana na Mbu waenezao Malaria katika Nyumba za na mazingira yanayowazunguka.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ahmed Makuwani alisema Serikali imepiga hatua katika kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwa maambukizi ya asilimia 8.1 tofauti na nyumba ambapo maambukizi yalikuwa zaidi ya marambili ya asilimia ya sasa.

Amesema, hatua hizo ni pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kwa zaidi ya asilimia sabini (70%) kutoka mwaka 2015 tofauti na sasa ambapo vifo vitokanavyo na Ugonjwa wa Malaria ni 3600 kwa Mwaka huku akiitaja mikoa yenye maambukizi makubwa ya Malaria kuwa ni pamoja na Tabora, Mtwara, Kigoma na Kagera.

Amesema Mikoa hiyo ina Afua mbalimbali za kupambana na mbu kutoka kwenye mazalia yake na kuhakikisha kuwa kunakuwa na unyunyuziaji wa ukoko kwenye majumba ya watu, matumizi ya vyandarua na kuhakikisha wanaopatikana kuwa na Ugonjwa huo wanapata Tiba Stahiki ili wasitengeneze mzunguko mwingine wa maambukizi toka kwa Mbu.

Awali mwakilishi wa Shirika la SWISS TPH linalo fadhiliwa na ubalozi wa Uswisi nchini, Noela Kisoka alisema wamekuwa wakitoa msaada wa kitaalam kwenye mambo mbalimbali yanayohusiana na Malaria, ikiwa ni pamoja na eneo la Udhibiti wa mbu, ufuatiliaji na tathmini pamoja masuala ya upimaji na matibabu ya ugonjwa wa malaria.

Aidha, alisema kuwa pamoja na afua hizo kuu katika mapambano dhidi ya Malaria Shirika hilo pia limejikita katika kusaidia masuala ya kisekta, kwa kuwa ugonjwa huo nchini unatakiwa kutokomezwa kwa ushirikiano wa pamoja wa sekta tofauti akitolea mfano sekta ya madini, ujenzi, kilomo n.k na kuongeza kusema kuwa sekta hizo zote zina jukumu la moja kwa moja katika kutokomeza ugonjwa wa Malaria.

Mikel Arteta kumrudisha Gabriel Heinze EPL
Watanzania waombwa AFCON 2027