Wakati mechi ya dabi ya Young Africans na Simba SC ikitarajiwa kupigwa kesho Jumamosi (Aprili 20), makocha wa zamani wa timu hizo Olivier Robert Robertinho na Nassredine Nabi wameichambua mechi hiyo kila mmoja akitoa maoni yake.
Young Africans inatarajia kuikaribisha Simba SC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni.
Young Africans ambao ndiyo wenyeji, msimu uliopita ilikuwa ikiongozwa na Nabi kabla ya kuondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Miguel Gamondi.
Nabi aliifikisha Young Africans kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini akaipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, kwa upande wa Simba SC ilikuwa chini ya Mbrazil, Robert Olivier Robertinho ambaye aliondolewa kwenye timu hiyo baada ya kuchapwa mabao 5-1 na Young Africans kwenye mzunguko wa kwanza na timu hiyo sasa ipo chini ya Abdelhak Benchikha.
“Young Africans haitakiwi kuidharau Simba SC, kwani ina hasira na matokeo ambayo wanayapata. Ni rahisi kwao kuja na nidhamu kubwa ya kuwazuia na wakifanikiwa, inaweza kuwa mechi ngumu.
“Faida iliyonayo Young Africans ni kuwa na kikosi ambacho kinaweza kuamua matokeo chenyewe, namheshimu kocha wao Miguel Gamondi, ameonyesha ni mzuri tangu achukue nafasi yangu klabuni hapo.”
“Simba Sc pia ina kocha mzuri Benchikha, anajua kucheza mechi kubwa, nadhani wachezaji wenyewe wataamua mchezo kulingana na hesabu za makocha wao, itakuwa mechi ngumu,” amesema Nabi Kocha wa FA Rabat ya Morocco.
Kwa upande wa Robertinho, amesema siku zote hakuna dabi rahisi.
“Simba SC ina wachezaji wenye mioyo migumu kama Kibu Denis, Fabrice Ngoma, Clatous Chama, na wengine hawa wanafahamu maana ya Dabi, hivyo wakiweka juhudi mbele wataibuka na ushindi kwenye mechi hii.
Young Africans ina timu bora ndiyo maana inapata matokeo mazuri, ni wazi itakuwa mechi ngumu kwani watakuja na morali kwamba walishinda mechi yao ya mwisho ya ligi lakini pia mechi yao ya mwisho dhidi ya Simba SC.” amesema Robertiho.