Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 TAMISEMI imepanga kukamilisha ujenzi wa maboma 6,415 ya miundombinu ya sekta ya afya na elimu kwa gharama ya Shilingi bilioni 183.63.
Mchengerwa ameyasema hayo wakati akijibu hoja za wabunge waliochangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Amesema kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 52.86 ni fedha za ruzuku ya serikali kuu na Shilingi bilioni 130.77 ni fedha zitokanazo na mapato ya ndani ya halmashauri na kuongeza kuwa, ukamilishaji wa maboma mengine utaendelea kadri ya upatikanaji wa fedha.
“Ninawalekeza makatibu tawala wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri kusimamia utekelezaji wa mwongozo wa uanzishaji wa maboma ili kuzuia uanzishaji wa maboma usiozingatia mwongozo na taratibu zilizopo,” Mchengerwa amesisitiza.
Mchengerwa ameanisha kuwa, Novemba mwaka jana Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilifanya tathmini na kubaini uwepo wa maboma 21,914 ya sekta ya elimu na afya yaliyoanzishwa bila kuzingatia mwongozo ambayo yanahitaji Shilingi bilioni 455.51 kwa ajili ya ukamilishaji.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo Mhe. Mchengerwa amesema, Serikali katika kipindi cha miaka mitatu 2020/21-2023/24 imetumia Shilingi bilioni 255.55 kwa ajili ukamilishaji wa maboma ya elimu na afya, ambapo jumla ya maboma 1,795 ya zahanati yenye thamani ya Sh bilioni 89.75 na maboma 12,700 ya sekta ya elimu yenye thamani ya Shilingi bilioni 165.8 yamekamilishwa.
Aidha, amewaagiza makatibu tawala wa mikoa na wilaya kusimamia miongozo ya uanzishwaji wa maboma ya wananchi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo ili kuwa na matumizi mazuri ya rasilimalifedha.