Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa amesema bila uhuru, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hawezi kutimiza ipasavyo wajibu wake wa kuhakikisha uwazi na uwajibikaji vinakuwepo katika matumizi ya fedha za Serikali.
Majaliwa amesema Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zinapaswa kutambua maeneo yanayostahili kutiliwa mkazo baina ya Serikali, Bunge, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi za Ukaguzi na Mabunge kwenye nchi za SADC (SADCOPAC).
“Miongoni mwa maeneo hayo ni kuunga mkono uhuru wa Ofisi ya CAG, bila uhuru, CAG hawezi kutimiza wajibu wake ipasavyo katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji wa fedha za Serikali, kwahiyo Wadau wote wanawajibika kulinda uhuru huu kupitia hatua za kisheria na msaada wa Taasisi zenu,” aliongeza Majaliwa.
Majaliwa alitoa kauli hiyo wakati akifunga Mkutano wa Kujenga Uelewa wa Pamoja na Ufanyaji wa Kazi wa Taasisi za Ukaguzi na Mabunge kwenye Nchi za SADC (SADCOPAC) uliofanyika kwa siku mbili , Visiiwani Zanzibar.
Amesema suala la kuimarisha uhusiano kati ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (AG) na Bunge ni la muhimu kwani linasaidia kurahisha utendaji kazi baina yao.
“Ushirikiano kati ya vyombo hivi unawezesha utendaji na usimamizi rahisi, unaruhusu uchunguzi mzuri zaidi wa matumizi ya fedha za serikali. Ushirikiano huu unaweza pia kuboresha utawala na uwajibikaji ndani ya Nchi Wanachama,” alibainisha Waziri Mkuu.