Serikali kupitia Tume ya Madini imefuta jumla ya maombi ya leseni 227 ambayo yamekosa vigezo vya kuendelea kufanyiwa kazi, kutokana na sababu ya kutolipiwa ada stahiki za maombi kwa mujibu wa Sheria pamoja na kukosa nyaraka zinazotakiwa kuambatishwa na maombi hayo

kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde hii leo Aprili 24, 2024 Jijini Dodoma wakati akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari na kusema uchambuzi uliofanywa na Tume ya Madini umebaini kuwa kuna watumiaji wa mfumo wa uwasilishaji maombi kwa njia ya mtandao wapatao 34 wanatumia mfumo vibaya kwa kuwasilisha maombi bila kulipa Ada stahiki.

Amesema, “mwezi uliopita Serikali ilipotangaza kufuta jumla ya maombi na leseni 2,648. wengi walidhani ni utani na Kuongeza kwamba, “nataka niwaambie Serikali hatupo tayari kuona watu wachache wanashikilia maeneo pasipo kuyaendeleza kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura ya 123.”

Waziri Mavunde amesisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais ya kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi na hivyo wale wote ambao hawapo tayari kufuata Sheria na taratibu za madini zilizopo hatafumbiwa macho.

Aidha, Waziri Mavunde ameeleza kuwa tangu alipotangaza kufuta leseni 2,648 mnamo tarehe 22 Machi, 2024 kumekuwepo na umakini mkubwa wa uwasilishaji wa maombi na kufanyika kwa malipo kwa mujibu wa sheria ambapo jumla ya mapato ya shilingi 2,430,647,335.99 yamekusanywa na Tume ya Madini, fedha hizo zimetokana na waombaji na wamiliki wengi wa leseni kuzingatia na kufuata taratibu za kulipia leseni na maombi yao kwa mujibu wa Sheria.

Katavi: Imani za kidini zasababisha mwili kufukuliwa uzikwe upya
Halmashauri kupimwa kwa ubunifu vyanzo vipya vya mapato