Swaum Katambo – Katavi.

Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi imeamuru mwili wa marehemu aliyefakamika kwa jina la Juma Andrea Bukuku  ufukuliwe na kuzikwa upya, baada ya mke wa marehemu kufungua kesi akidai mumewe alizikwa kwa imani ya Dini ya Kikristo badala ya dini ya Kiisilam.

Hali hiyo imevuta hisia za watu wengi na kusababisha taharuki katika mji wa Mpanda na Mkoa wa Katavi, baada ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Gasper Luoga kutoa hukumu hiyo kutokana na kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mdai Rehema Said, ambaye ni mke wa marehemudhidi ya mdaiwa Andrea Bukuku ambae ni baba wa marehemu.

Kesi hiyo, ilifunguliwa Mahakamani hapo kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 95 sura ya 33 ya mwaka 2019 na kifungu namba 9 cha Sheria ya uchunguzi wa maiti ambapo Rehema alifungua kesi ya kudai mwili wa marehemu mume wake Juma Andrea Bukuku uliozikwa kaburini ufukuliwe na uzikwe upya baada ya kuzikwa kwa imani ya dini ya kikristo badala ya dini ya kiislam.

Wakili wa mdai Hamad Arfi, alidai mahakamani hapo kuwa mwili wa marehemu unapaswa ufukuliwe na kuzikwa upya kwa kuwa marehemu alizikwa nje ya imani yake ya dini kwani kabla ya kifo chake kilichotokana na kugongwa na gari alifunga ndoa ya kiislam na mkewe Rehema huko mkoani Kigoma mnamo mwaka 2018.

Alisema, Rehema na mumewe waliendelea kukaa pamoja na marehemu huyo hadi mwaka 2022 ndipo walipotengana na licha ya kutengana waliendelea kuwa na mahusiano ya karibu kwa kuwa alizaa nae mtoto na pia hawakupeana talaka madai ambayo yalipingwa na wakili upande wa mdaiwa Patrick Mwakyusa aliyesema wanafahamu jina la marehemu ni Lwitiko Andrea Bukuku na si Juma Bukuku na kuwa dini yake ni mkiristo na alibatizwa katika Kanisa la Morovian.

Wakili Mwakyusa ameimbia Mahakama kuwa kwa maana hiyo Juma Bukuku na Lwitiko Bukuku ni watu wawili tofauti kwani marehemu wao kwa mujibu wa nyaraka walizo nazo zinaonyesha kuwa ni mkristo huku Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahaka ya Wilaya Mpanda Gasper Luoaga wakati akisoma hukumu hiyo akiiambia Mahakama kuwa marehemu baada ya kuwa mtu mzima alibadili dini na kufunga ndoa ya kiislam kwa kuwa alikuwa mtu mzima hakuhitaji ruhusa ya mtu yeyote.

Mahakama ilijiridhisha kuwa wakati marehemu anafunga ndoa huko Kigoma ndipo alipobadilisha jina na kuitwa Juma Andrea Bukuku na kuhamia kwenye dini nyingine ya kiislam na kutokana na ushahidi wa pande hizo mbili mahakama imetoa hukumu ya mwili wa marehemu kufukuliwa na kuzikwa upya kwa imani ya dini ya kiislam na kwenye ufukuaji huo wa mwili wa marehemu kuwepo na usimamizi wa karibu wa jeshi la Polisi na maofisa wa afya.

Hata hivyo, upande wa mdaiwa umesema utakata rufaa ya kuomba mwili huo wa marehemu kutofukuliwa na kuzikwa upya huku upande wa madai ukisema umeridhishwa na hukumu iliyotolewa kwani imezingatia sheria kwa kutambua marehemu alikuwa amezikwa kwa imani ya dini nyingine.

Marehemu Juma alifariki Aprili 15, 2024 na kuzikwa Aprili 17, 2024 katika makabuli ya Kashaulili yaliyopo Manispaa ya Mpanda kinyume na taratibu za Dini ya kiislam.

Wazalishaji mkaa mbadala kupatiwa ruzuku
Zoezi ufutaji wa maombi, Leseni kuwa endelevu - Mavunde