Naibu Waziri, Mwinjuma amesema Serikali imeandaa mkakati wa kuandaa timu si tu kwa ajili ya AFCON 2027, bali kwa mashindano mengine ambayo Tanzania itashiriki na zitagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100.
Amesema moja ya mkakati ni kutengeneza timu tatu za Taifa zitakazopishana umri ya kwanza itakuwa ni ya vijana chini ya miaka 17, itakayotokana na wanafunzi wa michezo ya UMISETA ya kila mwaka.
“Tukishawapata wachezaji hawa tutawaweka kwenye shule moja ambayo tumeshaiteua na watasimamiwa na walimu magwiji. Itapata mechi za mazoezi ya kutosha za ndani na nje. Kila mwaka wachezaji hao tutakuwa tunawapeleka kwenye akademi zenye mafanikio nje ya nchi ili kuendeleza vipaji tayari kulitumikia Taifa,” amesema
Mwinjuma amesema timu ya pili, itakuwa inayoundwa na vijana wenye umri wa chini ya miaka 23, ambao wanacheza ligi mbalimbali ndani na nje ya nchi na watakuwa wakikutana wakati wakiwa kwenye mapumziko ya timu zao.
Hata hivyo hakuweza kuitaja timu ya tatu baada ya kukatishwa na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kutokana na majibu kuwa marefu.
Kuhusu wasanii, Mwinjuma amesema Serikali imeandaa mkakati wa kuwashirikisha kwa kutunga nyimbo na utakaofanya vizuri ndiyo utakuwa wimbo rasmi wa mashindano hayo.
Katika swali la msingi, Mwanakhamis ametaka kujua mikakati ya Serikali ya kuihamasisha timu ya Taifa ili ifanye vizuri katika AFCON 2027 kama inavyofanyika kwa klabu za Simba na Young Africans.
Mwinjuma amesema Tanzania kwa kushirikiana na nchi za Kenya na Uganda itakuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027.
“Ili kuhakikisha timu ya Taifa inafanya vizuri katika mashindano hayo, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo ujenzi wa viwanja vya mpira katika majiji ya Dodoma na Arusha,” amesema
Amesema pia utafanyika ukarabati wa Viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru, na kuwatafuta na kuwaleta nchini wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaoishi na kucheza nje ya nchi ili kuchezea timu ya Taifa.
Naibu waziri amesema pia watahakikisha timu ya Taifa inashiriki mechi za kirafiki na mataifa mbalimbali na kufanya kambi katika mazingira mazuri ili kuwa na maandalizi bora.
Mwinjuma amesema mikakati mingine ni kuwashirikisha wadau wa michezo kuchangia timu za Taifa kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali fedha za kugharimia timu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa.
Amesema uenyeji wa mashindano ya CHAN mwaka 2024, ambayo ni maandalizi kwa timu ya Taifa kuelekea AFCON 2027 na kuajiri kocha na benchi la ufundi lenye sifa na uzoefu kwenye soka na kuhudumia timu zote za Taifa zinazoshiriki mashindano ya kimataifa.