Watanzania wanaojihusisha na mtandao wa kuwaingiza na kuwasafirisha wahamiaji haramu kwenda mikoa mengine na hatimaye kuelekea nchini Afrika Kusini kufanya kazi, wametakiwa kuacha mara moja tabia hiyo ambayo inaweza kuwaingiza matatani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo Mei 7, 2024 Afisa Uhamiaji Mkoa wa Tanga, Kagimbo Hosea amesema hali ipo shwari isipokuwa bado kumekuwa na wimbi kutokana na baadhi ya Watanzania ambao sio wazalendo wamekuwa wakitumika kwenye mtandao wa kuwaingiza wahamiaji haramu nchini.
Amesema “Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Tanga tumekuwa tukipambana kila wakati kuhakikisha tunautokomeza mtandao wa wahamiaji haramu, lakini kuna mawakala ambao wamekuwa wakitumika niwaonye waache mara moja kwani hawatasalimika pindi watakapokamatwa, tumekuwa tukitoa elimu lakini vitendo hivyo bado vinaendelea.”
Hosea ameongeza kuwa, mkakati wa Idara hiyo ni kuhakikisha wanadhibiti vitendo hivyo kwenye mkoa huo kwa kufanya vikao kwenye ngazi za Kata mbalimbali na kutoa elimu kwenye Vyombo vya Habari hususani radio, ili kudhibiti suala la wahaamiaji haramu.