Ili kuwajengea uwezo Wanafunzi mapema, Serikali imesema inatarajia kuboresha uelewa wa somo la Kiingereza kuanzia Shule za msingi darasa la kwanza, badala ya darasa la Tatu kama ilivyozoeleka tangu awali.
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu, TAMISEMI (Elimu), Dkt. Charles Msonde wakati akizungumza na Walimu wa Wilaya ya Chato na kusema moja ya maboresho ni pamoja na ufundishaji wa lugha hiyo na kuboresha mitaala.
Amesema, hali ya ufaulu wa somo la Kiingereza katika matokeo ya Darasa la Saba mwaka jana na mwaka juzi (2022/2023), siyo ya kuridhisha na ndiyo maana Serikali imeamua kuja na mkakati huo ili kuleta ufanisi.
“Ufaulu wa Wanafunzi waliofanya mtihani wa kitaifa wa Darasa la 7 mwaka Jana ni asilimia 34 kwa somo la Kiingereza wakati lugha hiyo ndiyo msingi wa ufundishaji wa masomo na lugha ya mawasiliano katika Shule za sekondari na matokeo ya mwaka 2022 ufaulu ulikuwa asilimia 29,” alisema Dkt. Msonde.
Afisa Elimu Mkoa wa Geita, Anthony Mtweve amewataka walimu wa wilaya hiyo kupokea maono, maagizo na maelekezo na kuzifanyia kazi, ili kupige hatua za kiutendaji na kuleta mabadiliko chanya.