Swaum Katambo – Tanganyika.
Zaidi ya wagonjwa 49 wa Mkoani Katavi wamepata huduma ya upasuaji wa matatizo mbalimbali kutoka kwa madaktari bingwa wa upasuaji wa Nchini Marekani, ambao wameweka kambi katika Hospitali ya wilaya ya Tanganyika.
Akizungumzia mafanikio tokea timu hiyo ya madaktari bingwa 17 ilipowasili katika Hospitali hiyo Mei 4, 2024, Daktari bingwa wa upasuaji kutoka shirika la Oparation International, Ravi Kothuru amesema licha ya kufanya upasuaji lakini pia wameshughulikia matatizo ya akinamama waliofika kujifungua.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amelishukuru Shirika la The Norbert & Friends Missions kwa kuamua kushirikiana na Halmashauri ya Tanganyika kupeleka huduma hizo, kwani imewapunguzia gharama za kifedha wananchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la The Norbert & Friends Missions, Joel Yalanda amesema kutokana ushirikiano walioupata kutoka Serikalini katika awamu zote mbili walizopeleka madaktari hao wataendeleza ushirikiano huo kwa kutoa matibabu na amesema shirika linakusudia kuanzisha kituo cha mafunzo ya madaktari bingwa katika Halmashauri hiyo.
Madaktari hao, watakuwa Hospitali ya wilaya ya Tanganyika hadi tarehe 10 mwezi huu wakitoa huduma za upasuaji bure ikiwemo upasuaji wa midomo sungura, makovu kuvu, ngiri, busha na uvimbe kwenye kizazi, matiti, mfumo wa chakula, kichwa na goita.