Kocha Mkuu wa Geita Gold, Dennis Kitambi amesema mambo ni magumu kwa timu hiyo kusalia kwenye Ligi Kuu soka Tanzania Bara msimu ujao.
Timu hiyo ilitoka sare ya bila kufungana dhidi ya Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Nyankumbu, mkoani Geita jana Jumanne (Mei 14) na kujiweka kwenye mazingira magumu ya kusalia kwenye ligi hiyo msimu ujao.
Matokeo hayo yanaifanya timu hiyo inayonolewa na Kocha Kitambi kufikisha pointi 25 kwenye mechi 27 na hivyo kuwa nyuma kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Tabora United inayoshika nafasi ya 14.
Kitambi amekiri timu yake kuwa na wakati mgumu kiasi cha kusalia Ligi Kuu msimu ujao kwani wamebakiwa na mechi tatu kati ya hizo dhidi ya Simba SC inayosaka nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini.
“Ukweli mambo ni magumu kwa timu yangu kubaki Ligi Kuu msimu ujao, tumebakiwa na mechi tatu na moja kati ya hizo ni dhidi ya Simba SC ugenini,” amesema Kitambi na kuongeza kuwa lipo tatizo kwa wachezaji wake kushindwa kutumia nafasi nyingi wanazotengeneza kwenye mechi.
Kwa upande wa Coastal, matokeo hayo yanaifanya kuendelea kujikita kwenye na fasi ya nne kwa kufikisha pointi 38 na hivyo kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) msimu ujao.
Mabingwa hao wa mwaka 1988 wa Tanzania Bara walicheza kwa nidhamu kubwa mchezo huo ambao wapinzani wao Geita walionekana kuhitaji zaidi matokeo kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao.