Makubaliano ya mkataba wa mwaka mmoja wenye thamani ya Shilingi milioni 150 ikiwa ni udhamini wa Wiki ya AZAKI 2024, itakayofanyika Jijini Arusha kuanzia Septemba 9 hadi 13, mwaka huu, yamesainiwa hii leo Mei 21, 2024 kati ya Shirika la The Foundation for Civil Society (FCS), na Vodacom Tanzania Foundation.
Akiongea katika hafla fupi ya kusaini makubaliano hayo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Justice Rutenge amesema kupitia wiki ya AZAKI, kiasi hicho cha fedha kimeongeza chachu ya ushiriano wa pamoja wa kukuza maendeleo ya jamii, ambapo FCS wamechangia shilingi milioni 250, huku michango mingine ikitoka kwa wadau wa maendeleo.
Amesema, “ili tuweze kusonga mbele na kuiona Tanzania tunayoitaka, sauti za wadau na wabia mbalimbali zinahitajika kusikika na ziwe sehemu ya kutoa mchango katika mchakato mzima wa maendeleo ambayo yatasaidia kujenga maono ya kulipeleka Taifa letu mbele.”
Rutenge ameongeza kuwa, Sekta Binafsi ni wabia na wadau wakubwa wa maendeleo, na ushirikiano huo ni muhimu katika kubadilishana uzoefu na kwamba FCS wamekuwa wabobezi wa zaidi ya miaka 20 katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Foundation Tanzania, Zuweina Farah amesema ili kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ushirikiano wa pamoja unahitajika kati ya AZAKi, Sekta Binafsi na Serikali na kuongeza kuwa lengo la Vodacom Foundation Tanzania ni kukuza ushirikiano, kuleta maendeleo ya jamii, kuimarisha utawala bora na kuboresha mazingira ya Biashara nchini.
Kauli mbiu katika Wiki ya AZAKI kwa mwaka huu (2024), ni ‘Sauti, maono na thamani’ ikiambatana na lengo Kuu la FCS la kuwezesha maendeleo ya jamii na Taifa kiujumla.