Uongozi wa Klabu ya Chelsea umetangaza kuachana na Kocha Mauricio Roberto Pochettino Trossero kwa makubaliano ya pande zote mbili ya kuvunja Mkataba ambao ulisainiwa mapema msimu wa 2023/24.
Kocha huyo alisaini mkataba wa miaka miwili, hivyo sehemu ya mwaka mmoja katika Mkataba wake ndio imevunjwa kwa makubaliano maalum yaliyofikia kati yake na Uongozi wa juu wa Chelsea.
Taarifa iliyosambazwa katika vyanzo vya habari ambayo imesainiwa na Wakurugenzi wa Michezo wa Klabu hiyo ya jijini London Laurence Stewart na Paul Winstanley imetoa shukurani kwa Kocha huyo ambaye amehudumu klabuni hapo kwa msimu mmoja.
Taarifa hiyo imeeleza: “Kwa niaba ya pande zote mbili, tungependa kutoa shukurani zetu kwa Kocha Mauricio kwa huduma aliyoitoa kwenye klabu yetu kwa msimu huu.
“Tunamtakia kila la kheri katika maisha yake nje ya Chelsea, tunaamini ipo siku huenda tukafanya naye tena kazi.”
Akizungumzia kuhusu kuondoka katika klabu hiyo, Pochettino amesema: “Sina budi kuushukuru Uongozi wa Chelsea kwa nafasi kubwa waliyonipa, nimekuwa sehemu ya historia ya Klabu hii,”
“Pia ninawashukuru sana Wachezaji wangu na Mashabiki ambao siku zote tulikuwa pamoja katika kipindi cha Raha na Simanzi, ninaitakia kila la kheri Chelsea katika mpango wake mpya.”
“Ninajivunia kuiacha klabu katika nafasi nzuri, Msimu ujao itashiriki Michuano ya Ulaya, hii imetokana na kazi kubwa niliyoifanya kwa kushirikiana na Wachezaji wangu hadi siku ya mwisho ya msimu, ninawapongeza sana kwa hilo.” amesema Kocha huyo kutoka nchini Argentina
Ushindi mara tano mfululizo mwishoni mwa msimu uliihakikishia Chelsea kucheza Michuano ya Ulaya msimu ujao, baada ya kumaliza nafasi ya sita kwenye Msimamo wa Ligi Kuu ya England.
Hata hivyo matarajio ya kuondoka kwa Pochettino yalikuwa makubwa kutokana na mwenendo wa kikosi cha Chelsea tangu alipokabidhiwa mikoba klabuni hapo mwanzoni mwa msimu huu.
Mbali na kuweweseka katika Michezo kadhaa ya Ligi Kuu, Pochettino alikiongoza kikosi cha Chelsea kufika Fainali ya Kombe la Ligi ‘Carabao Cup’ na Nusu Fainali ya Kombe la FA.
Uamuzi wa kuondoka kwa Kocha huyo mwenye umri wa miaka 52 uliripotiwa kufanywa baada ya mkutano wa siku mbili kati yake na viongozi Winstanley na Stewart, na mmiliki mwenza Behdad Eghbali.
Mwishoni mwa juma lililopita Pochettino alishiriki chakula cha jioni na Mmiliki mwenza wa Chelsea Todd Boehly, na hakuwa wazi kusema nini kilichojadiliwa kati yao, zaidi ya kusisitiza Chelsea itakuwa na muonekano mpya msimu ujao.