Sote tunafahamu kuwa kutokana na msongamano wa miji inayoendelea kukua hasa hii ya Kiafrika na ugumu wa maisha katika mifuko, ilipelekea wengi kuuona usafiri wa Bodaboda kama njia rahisi, nafuu na ya haraka kwa usafiri wa umma ambayo hata hivyo ina mambo mengi.

Kwa wasiofahamu Boda-Boda imepata jina lake kutokana na neno “mpaka”, kwani awali usafiri huu ulitumika kusafirisha bidhaa kati ya mpaka wa Uganda na Kenya ambapo zilikuwa zikisafirisha vitu mpaka kwa mpaka, na ilikuwa ni huko Busia mwaka wa 1988, zikiendelea kuenea katika miji kadhaa nchini Uganda na zikasoge maeneo mengine Afrika.

Changamoto za Bodaboda.

Nimewahi kupitia ukurasa wa Mabalozi wa Usalama Barabarani, RSA, hapo nilipata elimu iliyonijenga kwani ‘Admin’ wa kurasa hiyo alisema, kama Taifa bado hatujawa makini na utatuzi wa changamoto mbalimbali ama zinazosababishwa, ama wanazokabiliana nazo madereva wa Bodaboda.

Tumekuwa watu wa kukwepa tatizo hivyo anaona kuna uhitaji wa mkakati wa kitaifa kukabiliana na changamoto ya bodaboda na Bajaji nchini, kwani likizungumziwa tatizo la bodaboda wanaopelekewa lawama kwasasa ni Polisi na Halmashauri ambapo Polisi nao wakichukua hatua, humbling lawama.

Hatua hii imekuwa ikisababisha mapambano kati ya Polisi na Bodaboda au Bodaboda na Migambo wa Halmashauri na hii huwa ndogo pekee ya tatizo kwani Polisi na Halmashauri peke yao hawawezi kutatua au kupunguza changamoto ya Bodaboda zikaisha.

Anadhani ili tuweze kutatua changamoto ya bodaboda na Bajaj, ni lazima kubadili mitazamo na ili kubadili mitazamo hiyo kuna vitu lazima vitambulike.

Mambo ya kufahamu.

Kwanza ni ufahamu kuwa Biashara ya bodaboda na Bajaj ni halali tangu pale ambapo Serikali ilihalalisha usafiri huo miaka mingi iliyopita na hatimaye kutungwa kwa kanuni mwaka 2010, lakini jambo la pili ni kuelewa kuwa licha ya Kutungwa kwa Kanuni za Usafirishaji kwa Njia ya bodaboda na bajaji, sharti tutambue tatizo la bodaboda ni Zaidi ya kufuata masharti ya leseni pekee.

Jambo la tatu RSA wanasema Bodaboda ni sekta inayoajiri watu wengi wakiwemo wasomi kabisa wenye shahada ya kwanza na wasiosoma vidato kabisaa na la nne tujue kuwa Bodaboda ni sekta inayoendelea kukua na haitaondoka leo wala kesho.

Jambo la tano ifahamike kuwa wanaoongoza kutumia bodaboda ni pamoja na sisi wenyewe tunaowapiga marufuku tusipowahitaji na lile la sita ni kutambua changamoto ya bodaboda haitaisha kwa kuwaachia Jeshi la Polisi na Halmashauri peke yao.

Nini kifanyike.

Anasema kama tukienda kwa mtazamo huu, tutagundua kuwa kama taifa tunahitaji mambo ya kufanya ikiwepo mkakati jumuishi wa kushughulikia changamoto za bodaboda na bajaji kwa nchi nzima na nimuhimu Bodaboda na Bajaji wazingatiwe katika bunifu za barabara, ili nao wawe na njia za kupita kama ambavyo nchi zenye baiskeli nyingi zimetambua baiskeli kama usafiri rasmi na wakawawekea miundombinu.

Aidha, usafiri huu sasa uwe na kanuni maalumu zitakazohusishwa na sheria ya Usalama Barabarani na zile za Usafirishaji na pia mkakati huo uweke mfumo mzuri wa utambuzi wa Bodaboda na bajaji na kuwekeza miundombinu ya usajili kwenye kila Halmashauri.

RSA wanazidi kuelimisha kwa kusema maeneo ya mijini, Halmashauri zitenge maeneo ya kuegesha bodaboda na kuyawekea miundombinu kwani nje na hayo tutaendelea kuwa na mikakati isiyoeleweka kuhusu Bodaboda, huku tukitengeneza madhara kila uchao.

Ni sisi tuliruhusu kwa kuona kuwa usafiri huo ni halali. Ni sisi hao hao tukaanza kuupiga vita. Ni sisi wenyewe miaka kadhaa iliyopita tulisema bodaboda ni halali kufanya biashara popote mijini na hakuna kukamatwa na hawakukamatwa kweli na wakazoea.

Hitimisho.

Binafsi nionavyo mimi, Usafiri wa Bodaboda sio mbaya bali mifumo ya usimamizi wa usafiri huu ndio ina kasorozinazofanya uonekane mbaya.

Hakuna mfumo rasmi na rafiki wa kuwakagua madereva wa Bodaboda endapo wamekidhi vigezo vyabkuwa Barabarani na kuendelea na kazi hiyo ya usafirishaji, wengi hujifunza mitaani na baadaye kuingia katika soko kitu ambacho madhara yake kiukweli yapo wazi.

Nadhani kuwe na usajili wa vituo rasmi vya bodaboda na Madereva wawekewe utaratibu wa kupata mafunzo ya maalum ya uendeshaji salama ili kuepusha haya madhara ya mara kwa mara na kuwe na ukaguzi wa Madereva, pamoja na pikipiki katika vituo vyao vya kazi, na kwa yule asiyekidi vigezo asiruhusiwe kupakia abiria hadi pale atakaporekebisha kasoro zake.

Kwa upande wa abiria pia wawe na misimamo na wawekewe utaratibu hata wa vifungu vidogo vya sheria chini ya Mamlaka husika kwamba  wakatae kupanda abiria zaidi ya mmoja kwani udhibiti wa chombo hupungua kwa dereva akipakia abiria zaidi ya mmoja, hivyo ni rahisi kwenu kupata ajali endapo itatokea dharura.

Kusuhu lawama mara nyingi hupelekwa kwa Polisi pale inapotokea tatizo au ajali, lakini ikumbukwe tatizo hushikiliwa na muhusika, kama utakataa kupanda Bodaboda iliyozidisha abiria utaepuka mengi, kama utayoa taarifa za vihatarishi vya usalama ni wazi pia utaepusha mengi, tusiwape Polisi mzigo hili ni la kwetu sote.

Wanawake, Vijana kujengewa uwezo wa kibiashara
Iran: Simanzi yamuondoa Ayatollah msibani