Mchezaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Clement Mzize amewajibu baadhi ya Mashabiki wanaombeza hasa anaposhindwa kufikia lengo la kuisaidia timu yake, hasa anapopata nafasi za kufunga na kushindwa kufanya hivyo.
Mzize amekuwa Mshambulijai tegemeo kwa msimu huu 2023/24, baada ya kuondoka kwa Fiston Kalala Mayele aliyetimkia Pyramids FC ya nchini Misri, lakini ameshindwa kufurukuta, huku Aziz Ki akiongoza katika mbio za ufungaji Bora hadi sasa.
Mshambuliaji huyo mzawa amesema mara kadhaa amekuwa akisikia malalamiko ya baadhi ya Mashabiki kuhusu uwezo wake wa kutumia nafasi za kufunga, na wakati mwingine malalamiko hayo yamekuwa yakimpa chachu ya kujirekebisha.
Mzize amekiri kuwa na changamoto ya kukosa nafasi kadhaa za kukwamisha mpira wavuni na kuisaidia Young Africans kutoka Uwanjani ikiwa na idadi kubwa ya mabao, lakini bado akajitetea kwa kusema yeye si Mshambuliaji pekee duniani anayeshindwa kufanya hivyo.
Amesema Mashabiki hao baadhi wanapaswa kutambua kuwa, amekuwa akipambana sana kuisaidia Young Africans kuifungia mabao na inapotekea mambo yanakuwa tofauti wasimchukulie kama anafanya kusudi na kumtusi.
“Mimi sio Mshambuliaji pekee ninayekosa magoli, hata Ulaya wanakosa magoli pia, lakini kwa Watanzania ukikosa magoli wamekuwa watu wa kukutukana vibaya na hawaangalii huyu ni kama kijana ndio anachipukia, lakini niwaambie ujumbe wao kama nakosa sana magoli ninaupata sio kama siupati, na naufanyia kazi na Shabiki inawezekana ndio kocha wako namba moja” amesema Mzize