Swaum Katambo, Mlele – Katavi.
Mashuhuda wa ajali ya watu 7 kati ya 14 kuzama kwenye bonde dogo la maji katika Kitongoji cha Luguya kilichopo Kijiji cha Mwamapuli Wilaya ya Mlele mkoani Katavi wamesema chanzo cha ajali hiyo ni boti walilokuwa wamepanda kuzidiwa uzito.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko aliyefika kuwapa pole wamesema mtumbwi huo ulibeba abiria 14 pamoja na magunia 10 ya mpunga yaliyopelekea kuzidiwa uzito na kutumbukia kwenye maji.
Akizungumza kwa uchungu Nuhu Bahati amesema amepoteza ndugu zake wawili akiwemo mtoto wa miaka 14 ambao wanasadika pia kufariki kutokana na miili yao kutoonekana hadi sasa huku akisema ndugu zake hao walimwacha kambini kwa lengo la kuwahi kwenda kuchaji simu zao
Hata hivyo wameiomba Serikali kuangalia utaratibu wa kuziba kingo za mto Kavuu ambazo zimepelekea kumwaga maji na kusambaa katika mashamba ya wananchi wa Kijiji hicho.
Naye diwani wa Kata ya Mwamapuli, Edward Nyorobi amewataka wananchi kuchukua tahadhali kwa kutunza mazingira na kuepuka uharibifu wa mazingira hususani katika Mto Kavuu ambao ndio chanzo cha ajali hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amepiga marufuku wasafirishaji wanaotumia mitumbwi kubeba mizigo iliyozidi na kuweka abiria ndani yake huku akiwataka viongozi kusimamia kwa mujibu wa Sheria, kanuni na taratibu.
“Hata hii ukiitazama vizuri,gunia 10 kwenye mtumbwi pamoja na watu 14 kwa vyovyote vile chombo kinazidiwa nguvu naomba mjichunge wenyewe kwa kusimamiana kuhakikisha chombo kinabeba mzigo pekee bila kichanganya na abiria kwa idadi inayotakiwa,” amesema.