Sina shaka kila mtu anaupenda muziki iwe kwa kuimba au kucheza, lakini pia wengi wetu nina imani hakuna ambaye hajawahi kucheza muziki iwe kwa kujitingishika tu au kujaribu kuyumba yumba na kutelezesha miguu kama alivyokuwa akifanya bingwa wa Muziki aina ya Pop, Michael Jackson.

Lakini vipi ikiwa unacheza muziki halafu ukitaka kuacha kucheza inashindikana? yaani linapigwa sebene unainuka kulicheza unaanza  kusakata mauno, halafu ukitaka kuacha uendelee na ‘mishe’ zingine haiwezekani yaani inakuwa ‘show – show’ mwanzo mwisho haupoi.

Huenda hilo likawa ni jambo la kufurahisha na la kutafakarisha sana, lakini amini usiamini, limewahi kutokea na hali hii iliathiri mamia ya watu katika historia na ikapewa jina la Dance Mania au Homa ya Dansi.

Dance Mania.

Dance Mania ikaitwa kitaalam choreomania, na wengine wakasema ni Dance plague, yaani hamu ya kucheza dansi isiyoweza kudhibitiwa ambayo ilienea haraka katika jamii na katika baadhi ya matukio, vijiji kadhaa vilikumbwa na hali hiyo ya watu kucheza bila kupumzika.

Ilirekodiwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1021 W.K. katika mji wa Kijerumani unaoitwa Kölbigk. Walakini, hilo halitakuwa tukio la mwisho kwa katika karne chache zilizofuata, milipuko mingine iliripotiwa kote Ulaya lakini hasa ilikuwa ni Ujerumani.

Aidha, mlipuko huo mkubwa zaidi wa wazimu huo wa kucheza dansi ulitokea Aachen, Ujerumani mwaka wa 1374 na bila sababu au maelezo, watu walicheza kwa saa au siku nzima mfululizo wakicheza bila ala na kupita kiwango na walipochoka walikaanguka.

Ni nini kilisababisha.

Hilo bado ni fumbo. Wakati huo, watu wengi walielekeza kwenye vyanzo vya kiroho. Viongozi wa Kanisa walisema wacheza densi walikuwa wamepagawa. Wengine walidhani wamelaaniwa na watakatifu na hii ndiyo sababu wazimu wa kucheza wakati fulani uliitwa Ngoma ya Watakatifu.

Kesi za densi wazimu zilipotokea nchini Italia, waliziita tarantism. Waitaliano waliamini kuwa huenda ilisababishwa na kuumwa na buibui. Walifikiri kwamba dansi ya ajabu na miondoko ya mtetemo, ilikuwa ni hali ya mwili kujiondoa sumu ya buibui.

Walakini, wataalam wengi wa kisasa hupuuza maelezo hayo, wakiamini kuwa mvuto wa kucheza unaweza kuwa ulisababishwa na fangasi inayoitwa ergot, wakisema inaweza kuwa ilizalishwa katika mkate na kutoa sumu inayotengenezwa na fangasi na kusababisha maoni na mifadhaiko.

Majibu halisi yanakosekana.

Wengine wakasema hali hiyo huashiria mfadhaiko mkubwa wa kuishi katika enzi za kati. Kwa mfano, maeneo mengi ambayo yalikumbwa na wazimu wa kucheza pia yalishughulika na mapambano ya milipuko wa kitu kiliitwa Black Death, ambayo yalikuwa ni matukio ya vifo vilivyokosa majibu ya kusababishwa na nini.

Pia, iliarifiwa kuwa watu hao walikabiliwa na magonjwa mengine pamoja na njaa, wengi wao wakiwa chini ya shinikizo la viongozi wa Kanisa, ili waepuke matendo maovu na shughuli zinazoonekana kuwa chafu ikiwemo ya kucheza dansi.

Mtazamo wa wataalamu.

Wataalamu wengi waliamini kuwa wahasiriwa wa wazimu wa kucheza walikuwa wakiugua afya ya akili. Walidai wengine huenda walijiunga kwenye dansi kwa sababu si ya kuambukizwa, bali kwa msisimko mkubwa.

Hii ikawa ni moja wapo ya maelezo au sababu ambayo ilikubalika zaidi kutokana na hali hiyo ya ajabu kuwahi kutokea Duniani.

Habari njema.

Tukio hilo, linadaiwa ni moja ya yaliyowahi kutisha ulimwengu, yaani unachezaje bila kuacha mpaka uchoke na udondoke? Hata hivyo kuna habari njema pia kwamba hakujawahi kuwa na kesi zilizoripotiwa tangu katikati ya karne ya 17.

Watu wa leo ​​hawapati wazimu kama huo wa kucheza ingawa masharti mengine yanaweza kusababisha mtu kufanya jambo bila ya hiari yake, hivyo ukijikuta una dalili kama hii, mwambie mtu mzima unayemwamini ili aokoe jahazi.

Kucheza mpaka kifo.

Hata hivyo, Wazimu wa kucheza dansi au maarufu kama homa ya dansi iliathiri mamia ya watu kote Ulaya, inadaiwa katika milki ya Rumi dansi kama hilo lilitolea Julai 15, 1815 na hali hiyo ilidumu kwa mwezi mmoja wakicheza hovyo bila kuwa na uwezo wa kujizuia.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa, pia kuna wengine hawakuweza kuacha kucheza mpaka walipodondoka na kufa kutokana na uchovu. Hebu sema, wewe unafikiri nini kilisababisha hali hii? na ungefikiria kufanya nini ikiwa hali kama hiyo itarudi hii leo?…. hii ni Dar24 Media.

 

Ugomvi wa wanandugu wasababisha mauaji, wawili mbaroni
Usafirishaji: Miundombinu haikidhi mahitaji - Mrisho