Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini England Jack Peter Grealish huenda akachana na Mabingwa wa Soka wa Ligi ya EPL Manchester City, kufuatia madai ya kukiukwa kwa mkataba wake.
Grealish amekuwa hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha Manchester City, kama ilivyotarajiwa wakati akisajiliwa huko Etihad Stadium akitokea Aston Villa.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28, anatarajia kufanya mazungumzo na Kocha Mkuu Pep Guardiola, kuhusu mustakabali wake klabuni hapo ili kufahamu kama atarejea kwenye kikosi cha kwanza msimu ujao.
Gazeti la The Sun limeripoti kuwa Grealish amejipanga kuhoji muda wa kucheza ambao unaendelea kupungua kila kukicha, huku asilimia kubwa akitumika kama mchezaji wa akiba.
Hata hivyo Tovuti ya SunSport imeripoti kuwa miamba ya Ujerumani FC Bayern Munich wanafikiria kumsajilia winga huyo, endapo mazungumzo yake na Guardiola yatashindwa kuzaa matunda, ingawa inaelezwa kuwa Kocha huyo kutoka nchini Hispania bado ana nia ya kufanya kazi ya Grealish.
“Wanatarajia kukutana kwa ajili ya kuzungumza mambo kadhaa kuhusu mustakabali wa Grealish, kumekuwa na sintofahamu nyingi upande wa muda ambao amekuwa akitumika kiungo huyu.
“Grealish anaona hapaswi kutumika kama mchezaji wa akiba kwa mujibu wa mkataba wake klabuni hapo, awali mazungumzo kati ya wawili hao yalitarajiwa kuanza kabla ya mchezo wa Fainali ya Kombe la FA, ambapo Man City ilikubali kichapo cha 2-1 kutoka kwa Man Utd mwishoni mwa juma lililopita.” Imeeleza taarifa ya Gazeti la The Sun