Mkazi wa Sombetini Jijini Arusha, Peter Mwacha (18), ambaye ni Dereva wa Bajaji anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani humo kwa kukutwa akisafirisha dawa za kulevya bunda 316 zenye uzito wa kilogramu 98.55 pamoja na mtuhumiwa wa maujaji.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi mwandamizi wa Polisi, SACP. Justine Masejo imeeleza kuwa tukio hilo limetokea Mei 29, 2024 majira ya saa 08:22 mchana katika maeneo ya Elerai akitumia bajaji yenye namba za usajili MC 541 CXL aina ya TVS.
Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi Mkoani humo limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa mauaji Ramadhan Yahaya (28), maarufu kwa jina la Msambaa ambaye alihusika katika tukio la mauaji yaliyofanyika Mei 2024 eneo la Daraja mbili, Jijini Arusha.
Aidha, Kamanda Masejo amesema hali ya jiji la Arusha kwasasa ni shwari ingawa yapo matukio madogo madogo na wahalifu waliotenda wanaendelea kukamatwa kama alivyokamatwa mtuhumiwa huyo aliyekimbilia jijini Dodoma baada ya kutenda tukio hilo.
Hata hivyo, ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi Mkoani humo kwa kutoa taarifa za kweli za kihalifu kwenye vyombo vya dola au Serikali za mitaa, huku akiwataka kutokutoa taarifa kwenye mitandao zisizo za kweli akisema zinasababisha wahalifu kukimbia na kukwepa mkono wa sheria ikiwa ni Pamoja na kuleta taharuki na hofu kwa Wakazi na wageni wanaotembelea Mkoa huo.