Johansen Buberwa, Muleba – Kagera.
Watu wasiofahamika wamemuiba mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (2.5), katika Kijiji cha Bulamula kilichopo Kata ya Kamachumu Wilayani Muleba Mkoani Kagera, kisha kutokomea kusiko julikana.
Akizungumza na vyombo vya Habari
Mama wa mtoto huyo, Judith Richard amesema tukio la kuibiwa kwa mtoto wake limetokea nyumbani kwake Mei 30, 2024 majira ya saa moja na nusu usiku.
Amesema, mtoto wake Noela Asimwe Novath alimueleza kuwa walikuja wanaume wawili ambapo mmoja wao aliomba msaada wa chumvi na alipotoka nje alikabwa na watu hao kisha wakamchukua mtoto na kukimbia naye huku akiiomba Serikali kumsaidia ili aweze kupatikana.
Diwani wa Kata ya Kamachumu, Leodigad Chonde amesema tayari wameanzisha ulinzi shirikishi kwa kushirikiana na Jeshi la polisi wa kumtafuta kila sehemu ya Kata hiyo ili kuhakikisha mtoto huyo anapatikana akiwa hai.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Watu wenye ulemavu wa ngozi Wilaya ya Muleba, Mahamudu Musedemi amesema kitendo cha mtoto huyo kuibwa kinawafanya waishi kwa hofu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dkt. Abel Nyamahanga amesema Serikali inaendelea na zoezi la kuhakikisha mtoto huyo anapatikana na kuwataka Wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa jeshi la Polisi.