Swaum Katambo – Mpanda.

Wafanyabiashara wa viwanda vya kukoboa mpunga Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi wanafikiria kuvifunga viwanda vyao kutokana na kupungua kwa malighafi kwa kile wanachodai ushuru umekuwa mwingi na mkubwa kwa wakulima jambo linalopelekea wakulima wengi kushindwa kupeleka malighafi hiyo viwandani badala yake wanauzia mashambani na kukobolea vijijini.

Wafanyabiashara pamoja na wakulima, wanadai ushuru wa 2500 kwa gunia moja la mpunga ni mkubwa hivyo serikali ione namna ya kupunguza zaidi kama yalivyokuwa makubaliano yao katika moja ya kikao na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda.

Joyce Jackson, Ibrahim Madina na Donald Tarimo ni wawekezaji wa viwanda vya kukoboa mpunga Manispaa ya Mpanda, wameeleza suala la ushuru linapaswa kuangaliwa na kufanyiwa kazi.

Nao baadhi ya wakulima wa mpunga wamesema wanashindwa kusafirisha mpunga kuupeleka viwandani kutokana na ushuru mkubwa wanaotozwa jambo linalopelekea kuuzia vijijini kwa bei ya chini.

Kwa upande wake Benard Maige anasema katika kikao cha wafanyabiashara na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda yeye akiwa mwakilishi wa wafanyabiashara upande wa viwanda walikubaliana iundwe tume itakayokuja na suluhisho ya changamoto hiyo ambapo siku zimepita pasipo majibu.

Juhudi za kumtafuta Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda zinaendelea ili kutolea ufafanuzi wa jambo hilo ambalo linaonekana kikwazo kwa wamiliki wa viwanda vya kukoboa mpunga.

TCB yaiunga mkono Serikali utoaji huduma bunifu Kidijitali  
Kitabu cha Maadili: Kakulukulu ampongeza Sheikh Mkuu