Hati nne za Makubaliano zimesainiwa kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro kwenye kilele cha Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC), 2024 jijini Dar es Salaam, zikijumuisha Ushirikiano wa Kidiplomasia, Afya, Biashara na Viwanda na Teknolojia ya Habari.
Utiaji saini hati hizo umeshuhudiwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro anayeshughulikia Nchi za Kiarabu, Nchi zinazozungumza Kifaransa, Diaspora na Mtangamano wa Afrika, Mohamed Mbae.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo, Waziri Tax ameelezea umuhimu wa kusainiwa kwa hati hizo kuwa itawezesha pande hizo mbili kuwa na ushirikiano ulio katika mpangilio mzuri katika nyanja husika na hivyo kuleta tija zaidi.
“Pamoja na kutia saini Hati za Makubaliano pia tumekubaliana kuendelea kushirikiana katika maeneo mengine mengi ikiwemo miondombinu, nishati, ulinzi na usalama, uchumi wa buluu, utalii, utamaduni, sanaa na michezo na Maendeleo ya vijana,” alieleza Dkt. Tax.
Naye Mbae ameeleza kufurahishwa kwake na kufanyika kwa mkutano huo wa JPC na kuongeza kuwa mkutano huo ni kiungo muhimu katika kuendelea kukuza na kuimarisha uhusiano na kati ya Tanzania na Comoro.
Mbali na kusainiwa kwa Hati hizo Mawaziri hao wameridhishwa na kupongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa makubaliano na maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa kwa pamoja kati ya pande hizo mbili tangu kusainiwa kwa Mkataba wa Jumla wa Ushirikinao mwaka 2009.
Mkutano huo, umejadili na kuweka mikakati ya namna ya kuendelea kukuza biashara baina ya pande hizo mbili. Mikakati hiyo pamoja na mambo mengine italenga kuwahimiza sekta binafsi kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili na kuchangamkia fursa za kibiashara zilizopo na zile zinazotokana na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) na Eneo Huria la Biashara la SADC.