Mbunge wa jimbo la Bukombe ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kupendana na kuthaminiana ili kujenga Taifa imara.
Dkt. Biteko ameyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Msangila, Kata ya Runzewe Magharibi, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Amesema, katika jamii kuna mchanganyiko wa imani, hisia na tamaduni, lakini watu wote hukamilishwa na upendo, hivyo si busara watu hao kugawanywa kwa misingi ya chuki au tamaa ikiwemo vyeo na kadhalika.
Amewataka wana Bukombe kuvumiliana katika mapungufu yao, ili kujenga Tanzania imara na kuenzi msono ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye alipambana kuhakikisha Watanzanaia wanakuwa wamoja.
“Wote tuzungumze lugha moja.. Kiswahili ndiyo lugha yetu kuu kwa kuwa wote malengo yetu ni kuipeleka Tanzania mbele na maendeleo kwa mmoja mmoja. Hivyo tupendane bila kujali kabila, elimu, rangi au eneo la mtu anapotokea,” alisema Dkt. Biteko