Mhandisi Mshauri kutoka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini TARURA ambaye pia ni mratibu wa madaraja na barabara za mawe Falesi Elisha Ngeleja ametaja umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya madaraja na barabara za mawe katika ujenzi wa barabara, kuwa unalenga kupunguza gharama na kupata barabara imara katika kuwasaidia wananchi kuondokana na changamoto mbalimbali za usafiri.
Ngeleja ameyasema hayo katika maonesho ya ya Kimataifa ya Kilimo(Nanenane) yanayofanyika jijini Dodoma katika viwanja vya Nzuguni mkoani humo, wakati akieleza kazi ya TARURA, majukumu na umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya madaraja na barabara za mawe katika ujenzi wa barabara.
Amesema, katika maonesho hayo wamekuja na teknolojia ya kujenga madaraja na barabara kwa kutumia mawe kutokana na TARURA kuwa ni taasisi inayowawezesha wananchi hasa vijijini kufika sehemu zisizozifikika
“Maana yangu ni kwamba kuwawezesha wakulima kusafirisha mazao yao kutoka vijijini kwenda mpaka mjini na kusafiri kwa urahisi mara wanapopata changamoto ya kuugua wakati wanapokwenda kutafuta matibabu katika zahanati na vituo vya afya,” amesema.
Ngeleja ameongeza kuwa TARURA kutengeneza barabara na madaraka inawarahisishia wananchi Vijijini kutoa mazao yao kutoka mashambani mpaka sehemu ambapo kuna magari ili kusafirisha mazao hayo kupeleka sokoni.
Amesema, tangu TARURA ilipoanzishwa wamejenga madaraja 250 nchi nzima na mkoa wa Kigoma ndiyo unaoongoza, wakilenga kupunguza gharama za ujenzi na kufikia huduma kwa haraka madaraja yamejengwa kwa mawe mfano mikoa ya Mwanza, Kigoma, Morogoro ni baadhi ya mikoa iliyonufaika na teknolojia hiyo.