Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amezungumzia tukio la kutekwa kwa Allan Kiluvya, msaidizi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe akisema maelezo yaliyotolewa yanaibua mashaka.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamanda Mambosasa amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwani taarifa zilizotolewa na Allan na wazazi wake zinatofautiana.
“Kwanza tunaendelea na uchunguzi ili kubaini kwamba mhusika alitekwa… ukiziangalia clips zile, baba anasema mtoto amepigwa sana kwa sababu kulikuwa na tafrani, lakini mtoto aliposimama yeye anasema yeye ni mzima wa afya hajaumizwa na hajateswa,” amesema Kamanda Mambosasa.
“Lakini ukienda zaidi unaona anatoa ushirikiano na watekaji wamshushe wapi, wamshushe karibu na nyumbani. Kwahiyo ni watu marafiki, wanaoongea lugha moja. Kwahiyo, mashaka ni makubwa ndio maana sikulazimika kuisemea,” ameongeza.
Hata hivyo, amesema kuwa licha utata wa maelezo hayo, Jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kina kwa kutumia wataalam wake ili kubaini ukweli.
Saa chache baada ya kupatikana, Allan aliwasimulia waandishi wa habari kuhusu mazungumzo yake ya mwisho na wanaodaiwa kuwa watesi wake ambao walimtaka awaeleze ni wapi wakimshusha atakuwa salama.
“Wao wenyewe (Wanaodaiwa kuwa Watekaji) waliniuliza ni wapi tukikushusha unaweza kufika salama? Nikawauliza kwani tupo wapi? Wakasema tupo Gongo la Mboto. Nikasema mimi nakaa Kinyerezi mkinishusha njia panda ya Segerea nitakuwa salama,” alisema Allan.
Alisema kuwa aliripoti katika kituo cha Polisi na kwamba amewaachia waendelee na uchunguzi na kwamba atazungumza baada ya jeshi hilo kutoa taarifa ambayo ataona haiko sawa na alichowaeleza.