Februari 21, 1924 fundi seremala, Gabriel Matibiri na mkewe Bona walifanikiwa kupata mtoto wa kiume aliyeongeza idadi ya wanafamilia wa ukoo wa Zezuru ambao ni tawi dogo la kabila la Shona, Kusini mwa nchi ya Rhodesia Kusini ambayo sasa ni Zimbabwe.
Wanandoa hao waliokuwa wanafanya kazi kwenye kituo cha umishionari cha Roman Katoliki, walikuwa na watoto sita, na kati yao mzawa wa tarehe tajwa hapo juu walimuita ‘Robert’, ambaye baadaye aligeuka kutoka kudhihakiwa kuwa ni ‘muoga na ‘mtoto wa mama’ hadi kuwa Simba na Mwamba wa Afrika mwenye ujasiri wa kuwafurusha wakoloni weupe.
Ni Robert Mugabe, muasisi wa Taifa la Zimbabwe, mwiba ulioozesha miguu ya wakoloni na kufuta vumbi la ubaguzi wa rangi na utumwa wa fikra, ambaye leo ametangulia mbele ya haki akiwa na umri wa miaka 95.
Mugabe ambaye anafahamika zaidi kwa hatua yake ya kuwanyang’anya mashamba ‘wazungu’ na kuyarejesha mikononi mwa wazawa, alilelewa na kupata elimu yake ya msingi akiwa katika kituo cha wamishionari wazungu. Alipata nafasi ya kupata elimu kwa mwamvuli wa kazi aliyokuwa akifanya baba yake katika kituo hicho.
Akiwa shuleni, alitajwa kuwa mtoto mwenye tabia ya tofauti sana, alionekana kuwa ni mtoto msiri, aliyependa kusoma zaidi ya kucheza na watoto wenzake. Kutokana na tabia hiyo, alidhihakiwa kuwa ni ‘mtoto wa mama’ na muoga.
Katika miaka ya 1930, bundi alitua kwenye paa la familia ya Mzee Gabriel Mugabe. Mzee Gabriel alibishana na kiongozi wa kituo cha umishionari na kuonekana ni mtovu nidhamu. Hivyo, familia yake ilifukuzwa katika kituo hicho na kulazimika kuhamia katika eneo lingine kijijini hapo. Hata hivyo, watoto waliruhusiwa kuendelea na shule lakini wanapofunga wanarejea makwao, huko walikutana na maisha magumu kwani baba ambaye ni kichwa cha familia hakuwa na kazi tena.
Mwaka 1930, kaka yake Robert, Rafaeli alifariki dunia kwa ugonjwa wa kipindupindu. Baadaye, kaka yake mwingine, Michael alifariki kwa kile kilichoelezwa kuwa alikula mahindi yenye sumu kuvu. Siku chache baadaye, baba yake alikimbia familia akieleza kuwa anaenda mjini Bulawayo kutafuta kazi. Lakini baada ya muda, alianzisha familia nyingine huko mjini. Badala ya kurejea na pesa alizodai anaenda kuzitafuta alirejea kijijini na watoto wengine watatu.
Robert alifanya vizuri kwenye masomo yake na kufanikiwa kumvutia Padre Jerome O’Hea aliyeamua kumsomesha. Kwa bahati mbaya, kiongozi huyo wa kanisa alifariki mwaka 1970 akiacha maandishi yaliyomuelezea Robert kama mwanafunzi mwenye uwezo mkubwa wa kufikiria.
Baada ya kumaliza masomo yake, alipata nafasi ya kufundisha katika shule aliyokuwa anasoma huku akilipwa £2 kwa mwezi. Lakini baba yake alifariki dunia siku chache baadaye na kumuachia familia ya watoto watatu wa yule mama wa kambo wa mjini na ndugu zake wengine watatu wa mama mmoja, ambao wote walikuwa wakitegemea mshahara wa Robert (Mugabe).
Robert hakuchukua tabia ya baba yake kukimbia majukumu mazito yaliyoelemea mshahara wake mdogo hata kabla hajaanza familia yake mwenyewe, alipiga kazi akifundisha kati ya mwaka 1945 – 1960. Katika kipindi chote hicho, Mugabe alikuwa ameficha makucha, hakuwahi kuonekana katika masuala ya migomo dhidi ya wakoloni au hata kujihusisha na masuala ya siasa za nchi.
Huenda utulivu huo ndio uliosababisha aonekane mwema zaidi machoni mwa wakoloni, wakampa nafasi ya kusoma bure katika Chuo Kikuu cha Fort Hare nchini Afrika Kusini, hapo alisomea Shahada ya Masomo ya Historia na Fasihi za Lugha ya Kiingereza. Alipokuwa katika chuo hicho, Mugabe alianza kunoa makucha ya kisiasa. Alijiunga na chama cha siasa cha African National Congress na kuanza kujihusisha na harakati za mlengo wa Ujamaa akiamini katika Sera za mlengo wa Marxism.
Hata hivyo, alivutiwa zaidi na harakati za kiukombozi na sera za kiongozi wa Kiujamaa wa Kihindi, Mahatma Gandhi. Baada ya kuhitimu shahada yake ya kwanza, alielezea maisha ya chuoni hapo na elimu aliyoipata kuwa ndiyo siri ya mabadiliko makubwa katika maisha yake. Sasa akaachana na kuwa ‘mtoto wa mama’ na kuyaachia makucha ya kisiasa na kiukombozi aliyoyanoa chuoni hapo.
Aliporejea Zimbabwe mwaka 1952, alikuwa amevaa sura ya kuuchukia ukoloni na uonevu dhidi ya Waafrika. Alianza kazi yake kama mwalimu wa sekondari katika shule ya kimishionari karibu na eneo la Umvuma.
Kati ya mwaka 1955 hadi 1958, Mwalimu Mugabe alihamia Kaskazini mwa Rhodesia, akafanya kazi ya kufundisha katika chuo cha mafunzo ya ualimu cha Chalimbana. Huko alikutana na familia ya Emmerson Mnangagwa, akafanikiwa kumshawishi kujiunga na harakati za ukombozi, wakapambana bega kwa bega, na leo Mnangagwa ndiye Rais wa Zimbabwe akirithi kiti cha mwalimu wake kwenye siasa. Huenda hii ndiyo sababu wengi waliamini kujiuzulu kwa Mugabe na kumuachia Mnangagwa ni sawa na kugeuza upande wa sarafu lakini sio kuibadili sarafu.
Kiu na tamaa ya kuiona Rhodesia Kusini (Zimbabwe) ikiwa huru, ilimfanya avuke ng’ambo mwaka 1958 hadi nchini Ghana, wakati huo Ghana ilikuwa imeshapata uhuru na kuwa chini ya utawala wa Kwame Nkurumah. Huko ndiko alipokutana na mkewe ‘Sally Hayfron’. Kwakuwa mwanamke huyo alikuwa anavutiwa na siasa za ukombozi pia, alishibana na Mwalimu Mugabe hadi wakafunga ndoa.
Kweli kila mwanaume mwenye mafanikio, nyuma yake kuna mwanamke. Bi. Hayfron, raia wa Ghana alishikana mkono na Mwalimu Mugabe kufanikisha ndoto ya kuifanya Rhodesia kuwa huru kama ilivyokuwa Ghana.
Mwalimu Mugabe na mkewe waliitembelea Rhodesia Kusini mwaka 1960, wakati wa likizo yake. Alipofika, aliona mengi na akafanikiwa kukutana na mpigania uhuru Leopold Takawira ambaye aliwashawishi kuongeza muda wa kukaa nchini humo; na alifanikiwa kweli. Wawili hao waliongeza muda wa kukaa ambao ulibadilisha upepo wa maisha yao na kuandika historia mpya.
Siku chache baadaye, Takawira ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Chama cha Zimbabwe African Union, alikamatwa na Serikali ya Kikoloni.
Hapo ndipo kazi ya ukombozi ya vitendo ya Mugabe ilipoanzia. Alijiunga na kundi la watu 7,000 waliofanya maandamano kushinikiza Takawira aachiwe huru. Baada ya siku chache maandamano yalikuwa na watu zaidi ya 40,000. Kutokana na usomi wake, Mugabe alipewa nafasi ya kuzungumza kwenye kusanyiko hilo na alifanikiwa kuzigusa nyoyo za waanamanaji na kuwaongezea hamasa kuu. Mwitikio wa watu ulisababisha aache rasmi kazi ya kufundisha na kujiunga na harakati za ukombozi. Na mwaka 1961, alifunga ndoa ndani ya Kanisa la Roman Katoliki na Bi. Hayfron.
Hata hivyo, harakati za siasa mbele ya wakoloni hazikumuacha salama, alikumbwa na tuhuma mara kadhaa za uchochezi na alitupwa jela mara kadhaa kati ya mwaka 1963 na 1975. Wakati wote huo, alikataa kufuta kauli zake zilizodaiwa kuwa za kichochezi dhidi ya Serikali ya kikoloni na kutumikia kifungo jela.
Mugabe alifungwa kwa mara ya kwanza katika gereza lenye ulinzi mkali zaidi la Salisbury, akahamishiwa kwenye gereza la Sikombela na baadaye Que Que. Akiwa gerezani hakusahau kazi yake ya ualimu, aliwafundisha wafungwa waafrika hesabu, kiingereza na historia. Aliratibu madarasa yasiyo rasmi na kusambaza maarifa kwa wafungwa wenzake.
Kwa nia ya kulipa fadhira, wafungwa walisaidia kusafirisha kwa siri ujumbe wa Mugabe na wajumbe wengine wa kamati ya chama cha ZANU kwa wanaharakati nje ya gereza. Jumbe hizo zilisababisha kuundwa kwa kundi dogo la wapiganaji msituni huko Lusaka. Aprili 1966, walifanya jaribio la kwanza la mashambulizi dhidi ya Serikali ya kikoloni lakini lilishindwa. Serikali kwa kugundua hilo, ikawarudisha akina Mugabe kwenye gereza lenye ulinzi mkali zaidi na maisha magumu zaidi.
Alipotoka gerezani alikokaa miaka nane, alijiunga na kampeni ya vita ya msituni. Lakini baada ya rafiki yake wa karibu Maurice Nyagumbo kukamatwa, alitafuta maficho zaidi na akakimbilia Msumbiji.
Alikaa uhamishoni kwa miaka miwili nchini Msumbiji. Kiongozi wa Kijeshi wa Msumbiji, Samora Machel alikuwa na shaka juu ya Mugabe na alikuwa anasita kumtambua kama kiongozi wa ZANU. Lakini baada ya mwaka mmoja, alijiridhisha na kumtabua rasmi.
Akiwa Msumbiji, alitembelea kambi za jeshi na kufanya kazi kubwa ya kujenga uaminifu na ushawishi akitafuta kuungwa mkono na majeshi ya Zimbabwe African National Liberation (ZANLA), yaliyokuwa msituni na kutambulika kuwa yeye ndiye kiongozi wa mapambano dhidi ya Serikali ya kikoloni nchini Rhodesia Kusini. Mwaka 1977 alitangazwa rasmi kuwa Rais wa chama cha ZANU, na alitangazwa akiwa uhamishoni, Chimoio nchini Msumbiji.
Vikosi vya jeshi la ZANLA vilianza mashambulizi kutokea Msumbiji dhidi ya Serikali ya kikoloni ya Rhodesia Kusini. Takribani watu 30,000 wanadaiwa kupoteza maisha katika vita hiyo ya msituni. Mugabe alifanikiwa kushawishi Ubalozi wa China na kupata msaada wa kijeshi wa vifaa na silaha. Aliwafuata pia Korea Kaskazini na Cuba kwa Fidel Castro ambao walikuwa wana sera ya Ujamaa.
Mugabe alihamasisha mapinduzi dhidi ya Serikali ya Kikoloni, alitumia vyombo vya habari vya Msumbiji kuwahamasisha wananchi wa Rhodesia. Chama cha ZANU kiliungana na chama cha ZAPU kuhakikisha kinamuondoa mkoloni. Lakini mwaka 1976, alibaini mpango wa siri wa Nkomo wa ZAPU kutaka kufanya mazungumzo ya makubaliano na Serikali ya Kikoloni ambayo ni adui yao, mwaka 1978.
Hata hivyo, hakuwa na namna, msukumo wa nchi jirani ambazo ni marafiki wa Mugabe kutaka mazungumzo kati ya pande hizo mbili ulisababisha akubali kwa shingo upande kukutana na Serikali ya kikoloni jijini London nchini Uingereza. Walifikia makubaliano yaliyofahamika kama ‘Lancaster House Agreement’ ya mwaka 1979.
Hata hivyo, kwenye makubaliano hayo, Mugabe na Nkomo walikuwa na mitazamo tofauti ingawa walikuwa upande mmoja, Nkomo akikubali baadhi ya masharti ya kulegeza kamba kwa wakoloni, Mugabe aking’ang’ania kukaza uzi akitaka ukombozi wa bara la Afrika kwa sera za Kijamaa. Lakini mwisho wote walifikia makubaliano ya kuweka silaha chini.
Mwaka huo, ulifanyika uchaguzi mkuu wa kwanza, ZANU na ZAPU wote walijiondoa na haukupata utambuzi wa kimataifa.
Katika mkutano wa wakuu wa nchi za Commonwealth, Waziri Mkuu wa Uingereza wa wakati huo, Margaret Thatcher aliwashtua wengi baada ya kutangaza kuwa ataitambua Rhodesia Kusini kama nchi huru endapo tu watafanya uchaguzi huru na haki wa kidemokrasia kupata Serikali inayotokana na matakwa ya wengi.
Hata hivyo, baada ya kukubali kwa shingo upande makubaliano hayo kutokana na mashinikizo mbalimbali, mwaka 1980 Mugabe aliamua kushiriki uchaguzi mkuu kupitia chama cha ZANU-PF, akakataa kabisa wakati huu kuungana na ZAPU ya Nkome ambaye alimuona kama msaliti. Katika uchaguzi huo uliofanyika Februari 1980, ZANU-PF ilifanikiwa kupata asilimia 63 ya kura zote, ikishinda viti 57 kati ya 80 vya Bunge. ZAPU ya Nkome ilipata viti 20 tu na UNAC viti vinne.
Kutokana na matokeo hayo ya uchaguzi, alitangazwa rasmi kuwa Waziri Mkuu wa Rhodesia Kusini, na baada tu ya kuapishwa alitangaza kubadili jina la nchi hiyo kuwa Zimbabwe, jina lililotokana na sehemu ya kihistoria ya nchi hiyo ya zama za mawe iliyoitwa ‘Great Zimbabwe’. Miaka miwili baadaye alibadili mji mkuu wa nchi hiyo kutoka Salisbury na kuwa ‘Harare’. Lengo kuu lilikuwa kuibadili Zimbabwe kuwa na sura ya kijamaa.
Mwaka 1987, Bunge la nchi hiyo lilibadili Katiba ya Nchi, na Desemba 30 mwaka huo wakamtabua Mugabe kuwa Rais wa nchi, mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu. Lakini pia, mabadiliko hayo ya Katiba yaliweka viti 20 vya uwakilishi wa wazungu ndani ya Bunge.
Mkewe, Sally Mugabe raia wa Ghana akawa ndiye ‘First Lady’ wa kwanza. Alipendwa na alipewa jina la Amai yaani ‘Mama’. Kwa bahati mbaya, Sally alifariki dunia Januari 1992, kwa kile kilichoelezwa kuwa alipata tatizo la figo. Mugabe aliomboleza kifo cha mkewe hadi Agosti 17, 1997 alipofunga ndoa nyingine na Grace Ntombizodwa.
Katika kipindi hicho, amewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika. Hotuba zake kwenye majukwaa Umoja wa Mataifa (UN) zilikuwa maarufu na za kusisimua, zilizokosoa vikali mienendo ya nchi za Magharibi dhidi ya nchi za Afrika.
Tangu wakati huo, Zimbabwe ilifanya uchaguzi wa kidemokrasia mwaka 2000 ambapo Mugabe alipata ushindani mkubwa kutoka kwa Morgan Tsvangirai wa chama cha Movement for Democratic Change. Huo ndio mwaka ambao lilitokea sekeseke la kutaifisha mashamba ya ‘wazungu’ na kuwakabidhi wazawa.
Uchaguzi ukawa mzito, Tsvangirai akiungwa mkono na mataifa mengi ya Magharibi, akamtikisa Mugabe na ZANU-PF lakini hakufanikiwa kushinda uchaguzi.
Wawili hao walibaki kuwa washindani wakuu, hadi katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2008 ambapo Tsvangirai alipata kura nyingi zaidi ya Mugabe. Alipata 47.9% dhidi ya 43.2% za Mugabe. Huo ulikuwa uchaguzi uliozua mengi ikiwa ni pamoja na vurugu kubwa iliyoripotiwa kusababisha vifo vya maelfu. Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya nchi ilipaswa mshindi apate zaidi ya nusu ya kura zote. Hivyo, wakaunda Serikali ya mseto. Mugabe akaendelea kuwa Rais na Tsvangirai Waziri Mkuu.
Baada ya muda huo, Mugabe alishinda tena uchaguzi Mkuu na kuunda Serikali akiwa pia ni Mwenyekiti na muasisi wa ZANU-PF.
Joto la vuguvugu la mrithi wake kutokana na umri wake kuwa mkubwa lilianza kutikisa chama na taifa kwa ujumla. Mnangagwa aliyekuwa rafiki yake wa karibu na Makamu wake wa Rais, aliingia kwenye mgogoro na mke wa Mugabe, Grace.
Kuporomoka kwa hali ya uchumi, joto la kumpata mrithi wa Mugabe likazidi kuichoma ZANU-PF, ikasemekana kuwa Mugabe amepanga kumpa kijiti mkewe, Grace. Propaganda zikaeleza kuwa Mnangagwa anapanga pia kumpindua Mugabe.
Kutokana na maneno kuwa mengi, Mugabe akatangaza kumtimua Makamu wake wa Rais akidai ana njama ya kumuondoa Ikulu. Huko nje kukawa na maandamano makubwa ya wananchi wakipinga ugumu wa maisha na mfumuko wa bei. Uingereza na marafiki zao nao wakaweka ngumu kwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Zimbabwe. Jeshi, likaongoza waandamanaji na Mugabe akashauriwa kumwaga wino. Akakaza kamba kama kawaida yake. Bunge likatishia kumng’oa, akaona bora nikubali yaishe, kwa shingo upande, akamwaga wino wa kujiuzulu urais Novemba 21, 2017. Mnangagwa akatangazwa kuwa Rais Mpya na Mwenyekiti wa ZANU-PF.
Hadi umauti unamkuta Septemba 6, 2019 akiwa na umri wa miaka 95, ameliliwa na bara la Afrika kutokana na mchango wake mkubwa. Tanzania ni moja ya nchi rafiki zaidi kwa Zimbabwe na ina mchango mkubwa kupitia Mwalimu Julius Nyerere kwenye upatikanaji wa Uhuru wake.