Mamia ya wananchi mkoani Njombe na mikoa jirani wamejitokeza katika ibada ya kumuaga na mazishi ya mwili wa mwanasiasa Ibrahimu Kaduma aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje, Waziri wa Biashara na Waziri wa Mawasiliano katika serikali ya awamu ya kwanza ya mwalimu Nyerere pamoja na kushika nyadhifa mbali mbali hapa nchini.

Akitoa salaam za serikali katika ibada maalumu ya kumuaga marehemu Ibrahimu Juma katika kanisa la kiinjiri la kilutheri Tanzania Njombe mjini, mkuu wa mkoa wa huo Christopher Ole Sendeka amesisitiza mshikamano, maadili na uzalendo kwa watanzania ili kudumisha amani iliyopo pamoja na kuyaenzi yale yaliyoachwa na wanasiasa wakongwe wa taifa akiwemo marehemu Ibrahimu Kaduma aliyefariki agosti 31 mwaka huu nchini India.

“Tuendelee na umoja na maadili ambao baba alikuwa anausimamia,na kama kiongozi wa serikali naomba sana mipango yetu ya leo ndio itakayoamua Tanzania ya kesho,tukipanga vizuri na kusimamia hayo mema taifa letu litabaki kuwa salama na hayo ndio Ibrahimu Kaduma aliyasimamia”alisema Ole Sendeka

Nao viongozi mbali mbali wa dini walioshiriki katika ibada hiyo akiwemo askofu mkuu wa KKKT nchini dokta Fredrick Shoo, Askofu Alex Malasusa, Mchungaji Christopher Mwakasege wamesema marehemu mzee Kaduma katika uhai wake alisisitiza sana haki na maadili katika taifa na kuhimiza kuyaenzi yale mema aliyokuwa akiyapigania mzee Kaduma hasa katika suala la maadili ndani ya taifa.

“Ameacha mfano wa mtu muadilifu, mcha Mungu, mnyenyekevu na ametuachia mfano wa kuigwa pamoja na vyeo vyote kwa kweli hakuacha kumcha Mungu na kuwa mnyenyekevu”alisema dokta Fredrick Shoo

Makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania bara mzee Philip Mangula kwa niaba ya chama cha mapinduzi amesema kuwa mara nyingi mzee kaduma enzi za uhai wake alikuwa akilia na mmomonyoko wa maadili katika taifa hali iliyomfanya kuandika kitabu kinachohimiza haki na maslahi ya wananchi kama msingi wa maadili katika taifa.

“Katika mambo aliyokuwa akiyasema kwa uchungu sana maadili ya taifa letu yanamomonyoka tufanyaje kuyarudisha? kwa kweli maadili yanajengwa na taasisi mbali mbali yakiwemo makanisa haya ni wajibu wetu kuenzi haya yaliyoachwa na ndugu yetu”Alisema Mangula

Askofu mstaafu wa KKKT dayosisi ya kusini Isaya japhet Mengele amemuomba mkuu wa mkoa kufikisha salaam za kanisa hilo kwa rais na kwamba wapo pamoja katika ujenzi wa taifa huku akisisitiza serikali na vyombo vyake kuendelea kuwa makini katika kuwaokoa wananchi wake akiwekea mfano wa tukio la ajali ya moto ya lori la mafuta iliyoua zaidi ya watu 100 mkoani morogoro.

Mwili wa mwanasiasa mkongwe Ibrahim kaduma aliyeamua maisha yake kumkabidhi Mungu umepumzishwa katika nyumba yake ya milele huko Kibena Njombe ambako ndiko alikozaliwa mwaka 1937 hadi umauti ulipomkuta agosti 31 mwaka huu akiwa na umri wa miaka 82.

Mfahamu Mugabe, kutoka kuitwa ‘mtoto wa mama’, kufundisha wafungwa jela hadi kuwa Mwamba wa Afrika
Video: Kijana anayepumulia mashine nyumbani kuwekewa umeme bure