Mshambuliaji wa timu ya Simba Adam Salamba, ambaye amejiunga kwa mkopo na timu ya Al Jahra SC inayoshiriki Ligi Kuu nchini Kuwait, sasa ataanza kulipwa dola baada ya kusaini mkataba wa miaka mitano wa kuitumikia timu hiyo.
Salamba amesema moja ya mafanikio kuwahi kuyapata kwenye maisha yake ya soka ni kutimiza ndoto zake za kucheza nje ya nchi hivyo basi atahakikisha anaipeperusha vyema bendera ya Taifa.
“Nimesaini kandarasi ya miaka mitano huku Al Jahra ninaamini ni sehemu ya ndoto yangu ambayo nimeiota kwa muda mrefu, shukrani kwa viongozi wangu wa Simba, mashabiki pamoja na Serikali kwa sapoti yao licha ya kushindwa kuitumikia kwa muda klabu ya Namungo,” amesema Salamba
Kwenye mkataba wa Salamba wa sasa atapewa gari maalumu la kwendea mazoezini pamoja na la kutembelea pia atapewa nyumba yenye wafanyakazi huku mshahara wake ukiwa ni dola 4000 kwa mwaka na kila mwaka ataongezewa dola elfu moja.
Timu hiyo ya Salamba imeshiriki mara 21 kwenye Ligi Kuu nchini humo, ina taji moja la ligi ililolitwaa mwaka 1990 na inatumia uwanja wake Mubarak Al-Aiar.